Vitu Vinne Vinavyokufanya Usikamilishe Kazi Zako - Fahamu Hili
Saturday, April 20Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Vitu Vinne Vinavyokufanya Usikamilishe Kazi Zako

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kazi

Hakuna mtu anayependa kushindwa kukamilisha kazi au kitu alichokianza. Hata hivyo mara nyingi kutokukamilisha kazi hutokea kwa watu wengi.

Ni ukweli usiopingika kuwa zipo sababu kadha wa kadha zinazosababisha tatizo hili. Karibu nikufahamishe vitu vinne vinavyokufanya usikamilishe kazi zako.

1. Usingizi

Kuna usemi usemao “usingizi ni mlango wa umaskini”; kwa hakika kulala kupita kiasi ni jambo ambalo litakupotezea muda mwingi pamoja na ufanisi.

Unapolala sana unakosa muda wa kutosha kutimiza majukumu yako. Pia kulala muda mrefu hukufanya uamke ukiwa umechoka na kukufanya ukose ari na motisha wa kufanya kazi.

Soma pia: Njia 10 za Kuamka Mapema Asubuhi.

2. Intaneti na simu

Maendeleo yana manufaa yake na hasara zake. Kutokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano, watu wengi wamejikuta wakitekwa na teknolojia hii hadi kushindwa kutimiza wajibu wao.

Ni rahisi mtu kutumia saa mbili au zaidi kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Instagram au kutumia muda mwingi kuchati kwa simu ya mkononi.

Kwa hakika mambo haya ndiyo huwapotezea watu wengi muda ambao wangeweza kuutumia kukamilisha kazi yao. Hivyo ukitaka kukamilisha kazi zako hakikisha unatawala matumizi yako ya intaneti pamoja na simu.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda.

3. Kutokuwa na vipaumbele

Kwa hakika kuna vitu vingi vya kufanya kwa siku. Lakini ili uweze kuvikamilisha vyema huna budi kuweka mpangilio mzuri kwa kutegemea umuhimu kwa kila kitu.

Kuwa na vipaumbele kutakuwezesha kufahamu ni kazi ipi ianze na ifanyike kwa muda gani badala ya kufanya lolote linalokuja mbele yako.

4. Marafiki au wafanyakazi wengine

Inawezekana unafanya kazi kwenye ofisi au katika eneo ambalo umezungukwa na marafiki zako. Kwa njia moja au nyingine wafanyakazi wenzako au marafiki zako wanaweza kukuzuia kukamilisha kazi zako.

Kwa mfano ukiwa uko ofisini na ukaanza mazungumzo na mfanyakazi mwenzako, ni wazi kuwa utapoteza muda mwingi wa kazi.

Inawezekana pia una rafiki anayekushawishi kufanya mambo kama vile kumsindikiza kwenye matembezi au kukuingiza kwenye mazungumzo na shughuli nyingine ambazo hazihusiani na kazi zako.

Moja kwa moja unaona jinsi ambavyo unaweza kupoteza muda mwingi ambao ungeweza kuutumia kukamilisha kazi zako.

Neno la Mwisho

Ni muhimu kujifunza kusema hapana kwa mambo au watu ambao wanaweza kukupotezea muda na kukufanya usikamilishe lengo lako. Kumbuka kuwa kutumia muda vyema ni msingi wa mafanikio katika jambo lolote.

Soma pia: Faida 5 za Kusema “Hapana”.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kujiunga nasi kwa njia ya barua pepe au kwa kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

5 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x