Sababu 10 za Kwa Nini Baadhi ya Watu Wanafahamu Mambo Mengi - Fahamu Hili
Thursday, February 22Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Sababu 10 za Kwa Nini Baadhi ya Watu Wanafahamu Mambo Mengi

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Wanafahamu

Kwa hakika kuna watu ukiwatazama au kuwasikiliza unaweza kufikiri wana akili ya ziada. Maamuzi na ujenzi wao wa hoja ni wa hali ya juu sana.

Watu hawa wanajua mambo kwa undani na kwa usahihi. Ukiwauliza hiki au kile watakujibu bila wasiwasi tena hata na ziada yake. Naamini sote tunatamani kuwa kama watu hawa.

Je ni sababu gani zinawafanya watu hawa kufahamu mambo mengi? Karibu nikushirikishe sababu 10 zinazowafanya baadhi ya watu kufahamu mambo mengi zaidi kuliko wengine.

1. Wanasoma sana

“Fikiri kabla ya kuzungumza. Soma kabla ya kufikiri.”

Fran Lebowitz

Kusoma ni chanzo kimoja kikuu cha maarifa. Watu wanaojua mambo mengi husoma vitabu na makala nyingi kadri wawezavyo.

Hawasomi tu vitabu au makala, bali wanasoma vile ambavyo vina ubora na maarifa stahiki. Kwa njia hii wanafahamu mambo mengi na kuwafanya kutoa hoja zenye ushahidi na ufafanuzi wa uhakika.

Soma pia: Faida 15 za Kusoma Vitabu Unazotakiwa Kuzifahamu

2. Wanachangamana na watu

“Kwenye watu kuna mengi.”

Watu wanaofahamu mambo mengi wanapenda kuchangamana na watu pamoja na kujenga mtandao wa mahusiano. Watu hawa huhakikisha wanajenga mahusiano na watu sahihi hasa wale wanaofahamu mambo mengi.

Kwa njia hii wao nao hupata maarifa mbalimbali kutoka kwa watu wengine.

“Ukikaa na waridi nawe utanukia.”

3. Wanatazama na kusikiliza vitu vingi vya kuelimisha

Watu wanaofahamu mambo mengi wanatazama na kusikiliza vitu vyenye kuelimisha. Ni rahisi kumkuta mtu wa kawaida akitazama mziki au maigizo siku nzima; lakini watu wanaofahamu mambo mengi hawafanyi hivyo.

Watu wanaofahamu mambo mengi hutazama na kusikiliza vipindi au filamu mbalimbali zenye mafunzo ambayo yatawaongezea ufahamu na maarifa yao.

4. Wana shauku ya kujifunza

Huwezi kufahamu mambo mengi kama huna shauku ya kujifunza. Watu wanaofahamu mambo mengi hutamani kila mara kujifunza jambo jipya.

Hili huwafanya watafute maarifa na kutafiti juu ya mambo mbalimbali kila mara kwenye maisha yao.

5. Wanashiriki kwenye mijadala

Kushiriki kwenye mijadala hasa ya kisomi ni njia mojawapo ya kuongeza kiwango cha maarifa pamoja na uwezo wa kujenga hoja.

Watu wanaofahamu mambo mengi hushiriki kikamilifu kwenye mijadala mbalimbali na kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa watoa mada na washiriki.

6. Wanafundisha watu wengine

“Mwalimu ni mwanafunzi wa kudumu.”

Huwezi kuwafundisha watu wengine jambo ambalo wewe hulifahamu. Kwa njia ya kuwafundisha watu wengine, watu wanaofahamu mambo mengi hujifunza mambo mbalimbali kila siku ili waweze kupata maarifa ya kuwafundisha wengine.

7. Hushughulikia maendeleo yao binafsi

Ni watu wachache sana ndio wanafahamu umuhimu wa kuboresha au kujali swala la maendeleo yao binafsi. Watu wanaofahamu mambo mengi kila siku hutafiti na kutafuta mbinu na njia za kuwafanya kuwa bora zaidi.

Watu wanaofahamu mambo mengi hujishughulisha mambo kama vile kuongeza uwezo wao wa lugha, matumizi sahihi ya muda, kuboresha afya, kuongeza kipato, kuongeza ufanisi wa utendaji wao wakazi, n.k.

Kwa njia hii wanapata maarifa zaidi yanayowafanya kufahamu mengi na kuwa tofauti na wengine.

8. Huuliza maswali

“Asiyeuliza hana ajifunzalo.”

Kwa hakika asiyeuliza swali hana analojifunza. Watu wanaofahamu mambo mengi huuliza maswali mengi sana ili wafahamu mambo ambayo hawayafahamu.

Ikiwa nawe unataka kufahamu mambo mengi, niwazi kuwa ni lazima uulize kile usichokifahamu au kinachokutatiza ili uongeze wigo wako wa maarifa.

9. Hawaridhiki kirahisi

Kuridhika ni muhimu sana maishani, lakini kuridhika bila kitu hakuna maana yoyote. Watu wanaofahamu mambo mengi hawaridhiki kirahisi na yale wanayoyafahamu au vile walivyonavyo.

Watu hawa kila mara hutafiti na kuchunguza mambo mbalimbali ili kuongeza kiwango chao cha maarifa.

10. Wanasafiri sana

“Kutembea ni kuona mengi.”

Naamini umewahi kusikia kauli mbalimbali kamavile tembea uone mengi, mkaa bure si sawa na mtembea bure, n.k. Pasipo shaka, kauli hizi zinadhihirisha ukweli kuwa kutembea au kusafiri kuna manufaa mengi.

Watu wanaofahamu mambo mengi husafiri au kutembelea maeneo mbalimbali ili kujifunza mambo mengi zaidi. Kwa njia hii huwafanya wafahamu mambo mengi.

Neno la mwisho

Naamini sasa umeona ni kwanini baadhi ya watu wanafahamu mambo mengi kuliko wengine. Ni ukweli usiopingika kuwa kufahamu mambo mengi kunatokana na tabia yao ya kujiongezea na kutafuta maarifa kila wakati. Je wewe huwa unaongeza maarifa yako? Je unatumia njia gani?

Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini, kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kujiunga nasi kwa barua pepe hapo chini au kwa kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

3.3 3 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x