Njia 8 Rahisi za Kupunguza Matumizi ya Umeme - Fahamu Hili
Saturday, April 20Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Njia 8 Rahisi za Kupunguza Matumizi ya Umeme

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Matumizi hayaepukiki kwenye maisha lakini kubana matumizi inawezekana. Yapo mambo mengi ambayo hugarimu fedha ili kuyamudu yakiwemo huduma kama maji, umeme, gesi na mafuta.

Ni dhahiri kuwa ili kupunguza ugumu na changamoto za maisha ni vyema kujifunza namna ya kutumia vitu vyema.

Unaweza kuokoa fedha nyingi ambazo zingepotea kwa kulipia gharama zisizo na sababu za matumizi ya umeme. Hivyo fahamu njia 8 rahisi za kupunguza matumizi ya umeme.

1. Zima taa na vifaa visivyokuwa na uhitaji

Mara nyingi umeme mwingi hupotea kutokana na kuacha vifaa mbalimbali vikiwa vimewashwa bila sababu. Si jambo la kustajabisha watu kusahau taa za nje ya nyumba hadi saa sita mchana; au hata kuacha vifaa kama vile redio, televisheni au kompyuta vikiwa vimewashwa mchana au usiku kucha bila sababu ya msingi.

Jifunze kuzima taa na vifaa vingine vinavyotumia umeme wakati ambapo havihitajiki au havina umuhimu ili kookoa matumizi yasiyo ya lazima ya umeme.

2. Tumia nishati mbadala

Kuna watu hufikiri kuwa kutumia nishati kama vile umeme kupikia ndiyo kuwa wa kisasa zaidi; lakini ukweli ni kuwa huku ni kujiongezea gharama zisizokuwa na sababu. Matumizi ya gesi na umeme jua (solar) ni nafuu zaidi kuliko kutumia umeme kwa kila kitu.

Mambo unayoweza kufanya hapa:

 • Tumia gesi kupikia badala ya umeme kwani gesi ni nafuu zaidi.
 • Tumia taa na vifaa vya umeme jua (solar) pale inapowezekana.

Kwa kufanya hivi utaweza kuokoa nishati ambayo ingepotea katika matumizi ya umeme kwenye kila kifaa.

3. Ondoa vifaa vya zamani

Sera za dunia zimebadilika katika jitihada za kutunza mazingira. Vifaa vinavyozalishwa hivi leo, vingi hutengenezwa kwa kuzingatia kulinda mazingira kwa kuokoa matumizi ya nishati.

Hivyo ni vyema ukaondoa vifaa vya zamani kama vile televisheni, kompyuta za mezani, redio, taa au jokofu ambavyo vimetengenezwa kwa teknolojia ya zamani inayotumia umeme mwingi.

Mara ununuapo vifaa angalia vifaa vyenye nembo ya Energy Star ili kubaini vifaa ambavyo vimetengenezwa kwa kuzingatia kuokoa nishati.

4. Zima au punguza matumizi ya jokofu

Jokofu ni moja kati ya vifaa vinavyotumia kiwango kikubwa cha umeme. Kupunguza matumizi ya jokofu ina maana kuwa ni kubadili kiwango cha matumizi ya umeme.

Unaweza kuwasha jokofu kwa muda fulani tu na si kwa siku nzima; pia unaweza kuepuka kufungua jokofu mara kwa mara ili kutunza ubaridi ndani ya jokofu ili lisiwashwe mara kwa mara.

5. Tumia pasi vizuri

Ni vizuri kupasi kila nguo unayoivaa, lakini matokeo yake kwenye matumizi ya nishati siyo mazuri. Watu wengi hawafahamu kuwa umeme mwingi sana hupotea wakati wa kupasi na kuwasababishia kulipa bili kubwa za umeme.

Hata hivyo, yapo mambo unayoweza kufanya ili kuokoa matumizi ya umeme kwa kutumia vizuri pasi ya umeme.

 • Nunua pasi nzuri yenye viwango na ubora stahiki.
 • Nunua nguo zisizohitaji kupasiwa kila mara au kupasiwa kabisa.
 • Pasi nguo kwa pamoja. Ni vyema kupasi nguo tano kwa wakati mmoja kuliko kupasi kila siku nguo moja, kwani utapoteza umeme mwingi kupasha pasi moto mara kwa mara kila siku.
 • Usifue nguo kwa maji ya moto sana. Kufua nguo kwa maji ya moto sana husababisha nguo kujikunjakunja sana, hivyo kuhitaji umeme mwingi kuzinyoosha.
 • Pasia mahali sahihi. Unapopasia sehemu kama sakafuni ni dhahiri kuwa joto jingi litapotea kwa kupasha joto sakafu, hivyo kupelekea matumizi makubwa ya umeme. Ni vyema ukapasia kwenye meza maalumu ya kupasia au kwenye meza iliyofunikwa kwa kitambaa.
 • Pasi wakati kuna umeme wa kutosha. Inawezekana mahali unapoishi kiwango cha umeme hupungua wakati fulani; ni vyema kupasi wakati umeme upo wa kutosha ili pasi isivute umeme sana na kupelekea matumizi makubwa ya umeme.

6. Tumia taa zinazookoa nishati

Hivi leo sokoni kuna aina mbalimbali za taa  za umeme, lakini siyo zote zinafaa kwa matumizi yako. Balbu za zamani hutumia umeme mwingi zaidi huku zikikupa matokeo duni.

Leo zipo taa zinazojulikana kama “Energy Severs” ambazo zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia inayookoa nishati huku zikikupa matokeo mazuri zaidi.

7. Kagua mfumo wako wa umeme

Mfumo duni wa umeme (wiring) kwenye nyumba yako unaweza kusababisha upotevu mkubwa wa umeme. Kwa mfano ikiwa umeme unavuja kimakosa na kuingia kwenye waya wa aridhini (earth), umeme mwingi utapotea kwenda kwenye ardhi bila wewe kujua.

Unaweza kumtafuta fundi au mtaalamu wa masuala ya umeme wa nyumba, ili aweze kukusaidia kukagua mfumo wako na kuhakikisha kuwa hakuna sehemu inayovujisha na kukupotezea umeme.

Soma pia: Njia 10 za Kuepuka Majanga ya Moto Kwenye Nyumba

8. Tumia feni na kiyoyozi vyema

Mara nyingine kutokana na mazingira ya joto mtu anahitaji kutumia feni (pangaboi) au kiyoyozi ili kukabili joto. Ni vyema ukafahamu kuwa vifaa hivi huhitaji umeme ili kujiendesha; hasa kiyoyozi huhitaji umeme mwingi ili kufanya kazi.

Pamoja na hilo, yapo mambo kadhaa unayoweza kufanya ili kuokoa umeme unaotumiwa na kiyoyozi na feni.

 • Tumia njia za asili za kupambana na joto. Unaweza kufungua madirisha na milango kama inawezekana ili kukabili joto badala ya kutumia kiyoyozi na feni.
 • Unapowasha kiyoyozi funga madirisha na milango ili chumba kiwe na baridi haraka na idumu kwa muda mrefu zaidi.
 • Tumia zaidi feni kuliko kiyoyozi ili kupunguza matumizi makubwa ya umeme yanayotumiwa na kiyoyozi.
 • Zima feni na kiyoyozi pale ambapo havina ulazima.

Hitimisho

Ni dhahiri kuwa yapo mambo mengi yanayoweza kufanywa ili kuokoa matumizi ya umeme katika nyumba zetu. Ni wazi kuwa kubadili mtindo wako wa matumizi ya vifaa vya umeme, kila siku kutakuokolea kiasi kikubwa cha umeme kinachopotea bila sababu ya msingi.

Zipo njia nyingi inazopelekea kupotea kwa umeme lakini makala hii ilizingatia mazingira yetu ya kiafrika zaidi. Naamini sasa hutobeba tena gharama za umeme zisizokuwa na ulazima.

Soma pia: Njia 8 za Kuokoa Mafuta Unapoendesha Gari.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

3.2 5 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

4 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Alan BJ
Alan BJ
6 years ago

Ni dhahiri pesa nyingi zinapotea tu kuwalipa Tanesco; sasa nitawaweza;

Husna
Husna
4 years ago

Nimejifunza Jambo leo ,,lakini naomba nijue je rice cooker inatumika umeme mwingi au kidogo

Kornelio Maanga
Reply to  Husna
3 years ago

Asante sana kwa maoni yako ya thamani; inategemea ni rice cooker yenye uwezo gani, kama ni ndogo itakuwa inatumia umeme wa kawaida, vinginevyo iwe kubwa. Asante, karibu sana Fahamuhili.com

4
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x