Mambo 10 ya Kuzingatia Kabla ya Kununua Nyumba - Fahamu Hili
Friday, March 29Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kuzingatia Kabla ya Kununua Nyumba

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Nyumba

Kila binadamu anahitaji nyumba kwa ajili ya makazi. Kutokana na umuhimu wa nyumba, baadhi ya watu wamekuwa wakiamua kujenga nyumba zao wenyewe au kununua nyumba zilizojengwa tayari.

Hata hivyo, bado watu hawapati nyumba bora zinazokidhi mahitaji yao kutokana na sababu mbalimbali. Ni wazi kuwa ili upate nyumba bora kuna mambo ambayo unatakiwa kuyafahamu na kuyazingatia.

Ikiwa unataka kununua nyumba kwa ajili ya matumizi yako, basi fahamu mambo 10 ya kuzingatia kabla ya kununua nyumba.

1. Tambua mahitaji yako

Mara nyingi nyumba hujengwa kwa kutegemea mahitaji ya mmiliki. Hivyo kabla hujanunua nyumba bainisha mahitaji yako kwa nyumba husika.

Ikiwa unataka kuitumia kuishi basi hakikisha inakufaa, ikiwa pia unataka kuitumia kwa matumizi ya kibiashara, hakikisha inakidhi mahitaji hayo.

Ukinunua nyumba ambayo haikidhi mahitaji yako ni hasara kwani utahitajika kuirekebisha sana au hata kuivunja na kuijenga upya.

2. Fahamu gharama

Hakikisha kabla ya kuaamua kununua nyumba unachunguza gharama halisi za nyumba husika. Hakikisha gharama hizo unazielewa zote na unazimudu vyema.

Epuka kununua nyumba usiyoelewa gharama zake au kununua nyumba kwa madalali. Chunguza pia kama mmiliki wa nyumba ana deni lolote linalohusu nyumba husika ili lisije likakusumbua baadaye.

3. Fahamu ubora wa nyumba

Nyumba zinajengwa kila mahali lakini siyo zote hujengwa kwa kuzingatia kanuni za ujenzi bora.

Ni muhimu kukagua ubora wa nyumba unayotaka kuinunua ili usije ukapata hasara ya kupoteza pesa zako au kupatwa na ajali kama vile kuporomokewa na nyumba.

Soma pia: Makosa 8 ya Kuepuka Kabla na Wakati wa Kujenga Nyumba

4. Fahamu sababu ya kuuzwa kwa nyumba

Kuna wauzaji wa nyumba ambao siyo waaminifu, huuza nyumba mara inapokuwa inamatatizo au migogoro fulani.

Unaponunua nyumba yenye matatizo kama vile migogoro ya kisheria au umiliki, ni wazi kuwa utajitumbukiza kwenye matatizo makubwa.

Baadhi ya wamiliki wa nyumba wasiokuwa waaminifu huuza nyumba zilizowekwa rehani kwenye taasisi za kifedha na kuwasababishia wanunuzi wa nyumba hizo matatizo makubwa, hivyo kuwa makini kwa hili pia.

5. Nunua kwa kufuata sheria

Nyumba ni mali inayotambulika kisheria; kamwe usinunue nyumba bila makabidhiano ambayo yanatambulika pia kisheria.

Kamwe usimwamini mtu kiasi cha kukabidhiana nyumba kama vile mnakabidhiana kikombe cha chai. Hakikisha kuna nyaraka muhimu na hati zote zitakazokupa umiliki kamili wa kisheria wa nyumba husika.

Unaweza kumtumia pia mwanasheria aliye karibu nawe ili akupe ushauri au akusaidie kusimamia zoezi zima la kununua nyumba husika.

6. Fahamu eneo nyumba ilipo

Kuna watu wamenunua nyumba kwenye maeneo mabayo wanayajutia au kuyasikitikia kila siku. Nimeshuhudia watu wakinunua nyumba kwenye maeneo ya serikali, hifadhi maalumu, matindiga, au hata kwenye maeneo yenye migogoro ya kisheria na kujikuta wakipata matatizo lukuki.

Hakikisha unakagua vyema eneo ambalo nyumba ipo na uhakikishe ni zuri na linafaa kwa mahitaji yako.

7. Shirikisha wanafamilia

Ikiwa unafamilia, ni muhimu ukaishirikisha juu ya mpango wako wa kununua nyumba ili nao watoe maoni yao. Hakikisha kabla ya kununua nyumba husika hasa ya makazi, familia yako inaridhika na nyumba husika.

Kwa kufanya hivi utaondoa mivutano na misuguano isiyokuwa ya lazima kwenye familia yako. Pia utafanya familia ipende na ithamini nyumba husika uliyoinunua.

8. Fahamu uwepo wa huduma za kijamii

Je unataka kununua nyumba isiyokuwa na huduma kama vile maji, umeme au hata barabara ya kufika eneo husika?

Ni muhimu kuchunguza kama huduma za kijamii zinapatikana katika eneo nyumba ilipo, hasa kama nyumba ni ya makazi.

9. Fikiri kuhusu mbeleni

Mahitaji ya leo ya nyumba unayotaka kuinunua yanaweza yasiwe hivyo tena baada ya miaka mitano ijayo. Ni muhimu kuwaza mbeleni, ili ununue nyumba ambayo itakufaa kwa muda mrefu zaidi.

Kwa mfano kununua nyumba ya chumba kimoja wakati mnatarajia kupata watoto pamoja na wageni, huu siyo mpango mzuri.

10. Fikiri kuhusu kiwanja

Mara nyingi nyumba huuzwa pamoja na kiwanja. Ni muhimu ukafahamu kiwanja kinachohusiana na nyumba husika, je utahitaji kiwanja kikubwa kiasi gani sasa na baadaye? Je unalenga kutumia kiwanja husika kwa matumizi gani?

Ni muhimu pia kufahamu kama kuna gharama za ziada zinazousiana na kupata kiwanja mahali nyumba ilipo ili ufanye maamuzi sahihi.

Hitimisho

Kwa kuzingatia hoja zilizojadiliwa kwenye makala hii, naamini utaweza kununua nyumba bora kwa ajili ya mahitaji yako mbalimbali. Kumbuka kuzingatia utafiti wa kina kabla ya kufanya maamuzi ya kununua nyumba ili upate nyumba bora itakayokidhi mahitaji yako.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

3 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x