Kama unavyojua nembo au logo ya kibiashara ina nafasi kubwa katika utambulisho wa kampuni. Nembo iliyobuniwa vizuri inaweza kuwafanya watu wengi kutambua huduma au bidhaa unayotoa. Hii ndiyo sababu logo nyingi hupitia usanifu na maboresho mbalimbali ili kuhakikisha zinawakilisha kampuni au biashara vyema.
Hata hivyo, zipo logo zilizofanikiwa kufanya vizuri wakati nyingine hazijafanikiwa. Kwa zile zilizofanikiwa unaweza kushangaa ni kwa namna gani wabunifu wake wameweza kuficha maana fulani muhimu kuhusu kampuni husika.
Fahamuhili kwa kutambua umuhimu wa utambulisho katika biashara au kampuni, tumekuletea orodha hii ya nembo zaidi ya 10 pamoja na maana zilizojificha ndani yake. Tunaamini makala hii itakupa mwangaza muhimu pale utakapokuwa unatengeneza logo yako.
Soma pia: Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Kuchagua Jina la Biashara.
1. Toyota
Toyota ni kampuni mashuhuri ya kutengeneza magari. Nembo ya Toyota inavutia, kwani imejumuisha herufi zote za jina lake katika nembo husika. Je ulilifahamu hili? Unaweza kutazama hili katika picha hapa chini.
2. FedEx
FedEx ni kampuni ya usafirishaji ambayo ina nembo rahisi ukiitazama kwa haraka. Ukitazama kwa karibu nembo ya FedEx kati ya herufi “E” na “X” utaona mshale, ambao kwa hakika unamaanisha “haraka na kwa uhakika”.
3. Pinterest
Pinterest inalenga watumiaji wake kuweza kushikiza au kupini vitu mbalimbali kutoka kwenye mtandao kwenda kwenye ukurasa wa Pinterest. Ni dhahiri kuwa ndiyo sababu kitu kama kipini kimewekwa kwenye “P” pamoja na jina lenyewe kuwa “Pin..” yaani shikiza.
4. Amazon
Amazon ni duka au soko maarufu la kwenye mtandao. Logo yao ina mshale kwa chini unaoonyesha toka herufi “A” hadi “Z” wakimaanisha kuwa wana kila kitu unachokihitaji. Imekuwa ikitafsiriwa vibaya kuwa inamaanisha tabasamu “smile” lakini siyo kweli.
5. Sony VAIO
VAIO ni chapa ya Sony kwenye kompyuta pakato “laptop” wanazozizalisha. Alama ya VAIO siyo pambo bali inamaanisha kubadili mawimbi ya analogia kuwa ya digitali. Mawimbi ya analogia yamewakilishwa na “V” na “A”. wakati “I” na “O” vikimaanisha “1” na “0” ambazo ni tarakimu za kidigitali.
6. Cisco
Cisco inajulikana kwa kubuni, kuzalisha na kuuza vifaa vya mawasiliano. Hivyo si jambo la kushangaza kwa wao kuweka alama ya mawimbi ya kidigitali kwenye nembo yao. Alama hiyo ya mawimbi kwenye nembo yao pia inakaribia kufanana na daraja la “Golden Gate” lililoko San Francisco. Kwa njia hii Cisco wameweza kuonyesha wanachokifanya pia mahali walipo (San Francisco).
7. Picasa
Tovuti hii ya Google ya kuhariri na kusambaza picha haimaanishi tu jicho la kamera. Neno Picasa linasimama kuwakilisha “nyumba ya picha”. Casa ni neno la Kihispania linalomaanisha nyumba; ambapo ni dhahiri unaweza kuona umbo kama nyumba katikati ya nembo.
8. Formula 1
Formula 1 ni mashindano ya magari yanayofahamika pia kama F1. Katika nembo yao kuna F nyeusi pamoja na umbo jekundu likimaanisha kasi au mbio – lakini je, moja inatoka wapi? Tazama kwa karibu kati ya F na umbo jekundu utaona 1.
9. Cologne zoo
Hii ni nembo ya bustani ya wanyama ya Cologne; nembo hii haionyeshi tu kifaru na twiga kwenye umbo la tembo bali inaonyesha pia vinara vya kanisa kuu la Cologne Ujerumani.
10. Continental
Hii ni kampuni ya kuzalisha na kuuza magurudumu. Ukichunguza kwa karibu kati ya herufi “C” na “O” utaona umbo la gurudumu au tairi.
11. LG
LG ni kampuni maarufu ya kutengeneza na kuuza vifaa mbalimbali vya kielektroniki. LG wametumia “L” na “G” kwenye nembo yao ili kuunda umbo la uso. Pia wametumia rangi yekundu wakimaanisha urafiki. Hii inalenga falsafa yao ya ubinadamu na kujenga mahusiano mazuri na wateja wake ulimwenguni.
12. Gillette
Gillette ni kampuni maarufu ya kutengeneza vifaa mbalimbali hasa nyembe na vifaa vya kunyolea. Ukitazama kwa karibu utaona “G” na “I” vimekatwa kwa makali; hii ni kudhihirisha ukali (makali) ya nyembe na vifaa vyao vya kunyolea.
13. Unilever
Unilever ni nembo ambayo maana nyingi zimefichwa ndani yake. Ukichunguza kwa karibu nembo hii utaona bidhaa au shunguli mbalimbali za Unilever zikiwa pamoja na kuunda umbo la “U”. Ni dhahiri kuwa kwa haraka unaweza kuona matunda na vitu vingine vinavyohusiana na vyakula.
14. BMW
BMW ina historia ya kuanzia kwenye maswala ya ndege, na ni dhahiri kuwa nembo yao imetunza hili. Sehemu nyeupe inawakilisha pangaboi linalozunguka wakati sehemu ya bluu inawakilisha anga.
15. Wikipedia
Wikipedia ni kamusi au elezo huru maarufu sana duniani kwa sasa. Ni wazi kuwa ukitazama nembo ya Wikipedia utaona tufe lililotengenezwa kwa mchezo-fumbo (jigsaw) ambalo halijakamilika. Ni wazi kuwa nembo hii imebeba sera ya Wikipedia ya maarifa kwa kila mtu na kila mahali. Pia kukosekana kwa vipande katika tufe inamaanisha kuwa itakuwa ikiongezwa na kuboreshwa kila wakati.
Hitimisho
Hizi ni baadhi tu ya nembo ambao zimefanikiwa kuwasilisha ujumbe fulani au maana fulani inayohusiana na kampuni au biashara husika. Ni wazi kuwa umeona maana mbalimbali zilizofichwa katika nembo hizi. Ni matumaini yangu kuwa pia umeona na kufahamu jinsi ilivyo muhimu kutengeneza na kutumia nembo ambayo inaweza kutambulisha biashara yako kikamilifu.
Je una swali, maoni au mapendekezo? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
nashukuru mkuu nimekuelewa
Asante sana kwa maoni yako ya thamani Mkuu; karibu sana Fahamuhili.com
Naomba tuwasilianee 0744503476 Kuna kitu nahitaji kuongea na wewe
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Mawasiliano:
Email: fahamuhili[at]gmail.com
Simu: 0758 444 771