Vitu 10 Ambavyo Wazazi Wawajibikaji Wanavifanya - Fahamu Hili
Friday, September 29Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Vitu 10 Ambavyo Wazazi Wawajibikaji Wanavifanya

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Mzazi

Malezi ni swala linalohusisha pande kuu tatu, yaani wazazi, mtoto na jamii. Hivyo wazazi wanapaswa kuwajibika kusimamia nafasi yao ya malezi ya watoto ili watoto wao wakue kwenye misingi bora ya maadili.

Hili linatupa makundi mawili ya wazazi, yaani wale wanaowajibika na wale wasiowajibika katika familia na malezi. Ikiwa wewe ni mzazi au unatarajia kuwa mzazi, basi fahamu vitu 10 ambavyo wazazi wawajibikaji wanavifanya katika malezi ya familia zao.

1. Wanafanya kwa matendo kuliko maneno

Wazazi wawajibikaji wanafanya kwa matendo kuliko maneno, yaani wao kama wanawaagiza watoto wafanye kazi kwa bidii, nao utawakuta kila wakati wanafanya kazi kwabidii.

Ikiwa wanawahamasisha watoto wao kumcha Mungu au kuwa na maadili mema kwenye jamii, basi nao utawakuta wakiwa mstari wa mbele kuyatekeleza hayo.

2. Wanahamasisha kuliko kukosoa

Watoto wanahitaji kuhamasishwa kuliko kukosolewa, mzazi anayewajibika kila mara atajitahidi kumhamasisha mtoto wake kufanya mambo mbalimbali kuliko kumkosoa.

Wewe huwezi hili, hili umekosea, hujafanya vizuri, hutaweza kufanikiwa, hujui kitu, n.k. ni baadhi tu ya kauli za wazazi wasiowajibika kwani wao hukosoa kuliko kuhamasisha.

3. Wanatumia muda bora na watoto wao

Mihangaiko ya kutafuta kipato imeweka swala la malezi ya watoto kuwa kwenye hali mbaya. Wazazi wanaondoka watoto wakiwa wamelala wanarudi watoto wakiwa wamelala. Je mtoto atapata muda mzuri na wewe saa ngapi?

Wazazi wawajibikaji wanatenga muda bora kwa ajili ya kukaa na watoto wao ili wawasikilize, wawashauri au hata kuwatia moyo.

Soma pia: Makosa 15 ya Kuepuka Katika Malezi ya Watoto

4. Wanawajibika wenyewe

Uwajibikaji ni tatizo kwenye jamii ya leo; kamwe huwezi kuwa na mtoto anayewajibika kama wewe huwajibiki. Ni lazima mtoto aone ukijituma kwa juhudi, moyo na kwa nguvu zako zote kutimiza wajibu wako.

Ukiwajibika wewe kama mzazi hata mtoto atawajibika kwani anaona unavyojituma wewe mwenyewe kutafuta pesa na mahitaji ya familia bila kusukumwa na mtu yeyote.

5. Wanazungumza na watoto wao

Baadhi ya wazazi hufikiri kuwa hakuna kitu cha maana wanachoweza kuzungumza na watoto wao. Kama nilivyotangulia kusema, kutokana na mihangaiko mingi wazazi wengine hawana muda kabisa wa kuzungumza na watoto wao.

Wazazi wawajibikaji wanafahamu umuhimu wa kuzungumza na watoto wao, hivyo hawalipuuzii swala hili.

6. Wanaelewa lugha ya upendo ya watoto wao

Watoto wana lugha yao, tena lugha inayotakiwa kujaa upendo. Wazazi wawajibikaji hawaongei na watoto wao kama mdai na mdaiwa au kwa kutumia lugha za matusi na ukatili.

Wazazi wawajibikaji huwaonyesha watoto wao upendo kwa kuzungumza nao kwa lugha yao ya upendo.

Soma pia: Maneno 20 Ambayo Hutakiwi Kumwambia Mtoto Wako

7. Wanaruhusu watoto wao kufanya maamuzi

Wazazi wengi hupenda kuishi ndani ya watoto wao au kutaka watoto wao waishi ndoto zao. Kama wewe mzazi ulishindwa kuwa daktari basi usimlazimishe mtoto awe daktari.

Mpe uhuru wa kufanya maamuzi katika maswala mbalimbali ya maisha yake ya sasa na ya baadaye. Jambo la kuzingatia ni kumsaidia kufanya maamuzi bora na kuyasimamia ili yatimie.

8. Wanahimiza maadili kuliko vitu

Wazazi wawajibikaji kila mara husisitiza maadili mema kabla ya vitu. Mtoto hata avae vizuri au awe na maksi nzuri shuleni kamwe hawezi kufika mbali kwani tabia mbaya zitamwangamiza.

Ikiwa wewe ni mzazi basi ni muhimu sana kuhamasisha maadili kuliko vitu ambavyo vinaweza kuharibika mara moja.

9. Wameshikamana wao kama wanandoa

Wazazi walioshikamana ni lazima na watoto wao watashikamana. Ili kuonyesha mfano mzuri kwa watoto ni lazima wazazi washikamane vyema kwenye kila jambo na maamuzi mbalimbali.

Wazazi wawajibikaji hawaonyeshi kutengana au kutofautiana kwa namna yoyote mbele ya watoto wao. Hata jambo lisipokwenda vizuri wao hulimaliza wenyewe ndani kwa ndani.

10. Hawaruhusu teknolojia iwatawale watoto

Teknolojia imekuwa na manufaa makubwa sana lakini pia imekuwa na athari nyingi sana hasa kwenye swala la malezi ya watoto.

Badhi ya wazazi hufikiri kuwa kumnunulia mtoto televisheni, simu au kompyuta ya bei ni kumsaidia sana; lakini ukweli ni kuwa vitu hivi vinapaswa kutawaliwa vyema visije vikaharibu maadili ya mtoto.

Wazazi wawajibikaji wanafahamu vyema swala hili. Hivyo hawaruhusu teknolojia kuwatawala watoto wao au kuathiri maadili yao.

Soma pia: Vitu 10 Vinavyoharibu Maadili ya Watoto

Hitimisho

Naamini umeona jinsi ambavyo wazazi wawajibikaji wanavyowajibika kuhakikisha malezi ya watoto pamoja na familia zao yanakwenda vyema. Ni wazi kuwa wazazi kuwa mfano mwema ni muhimu sana kama wazazi wanataka kupanda mbegu njema kwa watoto wao.

Je una maoni au swali lolote? Tafadhali toa maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Pam
Pam
10 months ago

Asante sana nimekifunza kiti

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x