Makosa 15 ya Kuepuka Katika Malezi ya Watoto - Fahamu Hili
Tuesday, March 19Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Makosa 15 ya Kuepuka Katika Malezi ya Watoto

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Malezi ya Mtoto

Swala la malezi ya watoto ni swala nyeti, pana, gumu, na lenye changamoto nyingi; hivyo linahitaji umakini mkubwa na maarifa stahiki.

Kutokana na umuhimu huu basi, ni wazi kuwa changamoto au matatizo mengi ya kimalezi yanayotokea kwenye maisha ya watoto yanatokana na makosa yanayofanywa na wazazi katika malezi.

Pamoja na kwamba hakuna kanuni ya malezi, lakini yapo makosa ambayo wazazi wanapaswa kuyaepuka katika swala la malezi ili kuhakikisha watoto wao wanakuwa katika maadili na misingi sahihi.

Karibu nikufahamishe makosa 15 ambayo kila mzazi au mlezi anatakiwa kuyaepuka katika malezi ya kilasiku ya watoto.

1. Kumfurahisha mtoto

Kumfurahisha mtoto ni muhimu kufanywa na kila mzazi au mlezi, lakini ni lazima kuwe na kiasi. Wazazi wengi wamekuwa wakifanya kosa la kutaka kuwafanya watoto wao wafurahi kwa kila kitu. Mtoto akitaka hiki anapewa au akitaka kufanya hivi anaruhusiwa alimradi tu awe na furaha.

Kwa kosa hili unatengeneza mtoto ambaye hatokuja kuambilika mbeleni; atakuwa huku akifahamu kuwa kila anachokitaka ni lazima akipate na kikubaliwe.

2. Kumwabudu mtoto

Watoto wameumbwa na Mungu kupendwa na si kuabudiwa. Mtoto akifahamu kuwa unamwabudu, atakuendesha na kamwe hatokutii kwani anafahamu kuwa yeye ndiye anayetawala moyo wako.

Pia si vyema kumwabudu mtoto kwani mara apatapo shida kama vile kifo, utakuwa kwenye hali mbaya kwani imani na moyo wako wote uliuweka kwake.

3. Kujadili na kudharau wazazi na watoto wengine

Kuna wazazi wana tabia ya kuwajadili na kuwadharau wazazi na watoto wengine mbele ya watoto wao. Hili ni jambo baya sana kwani linawajengea watoto tabia ya dharau na kuwasengenya watu wengine.

Tambua mtoto ni sawa na karatasi nyeupe inayoandika mambo mbalimbali; hivyo unapoonyesha tabia mbaya mbele ya mtoto ataishika moja kwa moja.

4. Kuwafundisha kuishi kwa sheria

Kuna familia nyingine ukifika utafikiri ni kambi ya jeshi; watoto wanaishi kwa sheria kali na ngumu. Kuwalea watoto kwa sheria hakuwafanyi kuwa bora bali huwafanya waigize nidhamu na pindi wawapo nje ya nyumbani watavunja sheria zote.

Nimeshuhudia watoto waliowekewa sheria ya kutokunywa pombe au kuvaa nguo za ovyo nyumbani, lakini wawapo nje ya nyumbani huvunja sheria hizo hadi kupitiliza.

Ni muhimu ukamsaidia mtoto kutambua yeye mwenyewe umuhimu wa kuishi katika maadili kwa ajili ya badaye yake na si kumlazimisha kuishi kwa sheria.

5. Kuwalazimisha kushika imani kwa nguvu

Hakuna mzazi asiyependa mtoto wake awe mtu wa imani. Lakini tatizo linakuja juu ya ni kwa njia gani wazazi wanawawezesha watoto wao kushika imani.

Mzazi anapomlazimisha mtoto kushika imani, moja kwa moja mtoto ataiacha imani hiyo atakapokuwa mbali na mzazi; ni muhimu kumfanya mtoto atambue umuhimu wa imani yeye wenyewe na si kwa kumlazimisha. Hata hivyo unaweza kufanya haya yafuatayo kama mzazi:

  • Kuwa mfano wa kuigwa katika imani. Usimlazimishie imani ambayo wewe mwenyewe huna.
  • Mwonyeshe faida za kuishi kwenye imani.
  • Mwonyeshe athari za kuishi bila imani.
  • Mpe rasilimali zote zinazohitajika katika imani.
  • Fanyeni matendo ya kiimani pamoja katika familia (Kuomba, kusoma maandiko ya imani yenu, kujadili kwa pamoja maswala ya imani n.k.).
  • Mpongeze pale anapofanya jambo zuri la kiimani.

Kwa njia hii mtoto wako atakuwa katika misingi bora ya imani ambayo hataiacha.

6. Kutokuwa na muda wa kuwasikiliza

Wazazi wa leo kwa lugha ya mtaani wako “bize” kutafuta pesa na hawana muda na watoto. Ikumbukwe kuwa watoto nao wanahitaji kusikilizwa.

Mara kadhaa umewahi kusikia watoto waliojiua au kujidhuru kutokana na kuwa na matatizo ambayo walikosa mtu wa kumweleza. Hakikisha hata kama una shughuli nyingi kiasi gani hukosi muda wa kukaa na kumsikiliza mtoto wako.

8. Kugombana mbele ya watoto

Kuna wazazi wasiokuwa na staha kabisa, wao hutukanana na hata kupigana mbele ya watoto wao. Mtoto anapoona wazazi wakitukanana na kupigana, huiga tabia hiyo na kwenda kuifanya kwa wenzake na hata kwenye ndoa yake ya baadaye.

Ukiwa kama mzazi unayempenda mtoto wako, basi hakikisha tofauti zenu mnazimaliza kwa hekima na busara, tena ikibidi chumbani kwenu ili watoto wasipate mbegu mbaya kutoka kwenu.

9. Kuruhusu utamaduni wa kimagharibi uwatawale

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameingia mpaka kwenye swala la malezi. Wazazi wengi wa karne ya 21 wameruhusu watoto wao  kutawaliwa na utamaduni wa kimagharibi.

Kwa mfano unamwekea mtoto televisheni yenye chaneli za kiasasa ua unamruhusu kutumia intaneti ya kawaida ambayo haijachujwa kwa ajili ya watoto. Ni wazi kuwa mtoto atajifunza tabia za ajabu ajabu kutoka kwenye tamaduni za kimagharibi zilizoporomoka.

Hata hivyo unaweza kufanya haya yafuatayo:

  • Usiruhusu mtoto wako kutumia televisheni au mtandao kwa muda mrefu.
  • Tawala chaneli na vipindi ambavyo mtoto wako anavitazama.
  • Tawala intaneti ya mtoto. Unaweza kumfungulia mtoto injini pekuzi (search engines) kama vile http://www.kidrex.org/ na https://www.kiddle.co/ ambazo zinachuja maudhui salama kwa watoto.

10. Kuwa mkatili kwa mtoto

Naamini mara kadhaa umewahi kusikia mzazi amempiga mtoto hadi kufa au kumfanyia ukatili mwingine kwa kigezo tu kuwa mtoto amekosea.

Ni vizuri ukafahamu kuwa mtoto huonywa kwa hekima na upendo ili atambue kosa lake na afahamu kwanini ameadhibiwa ili asirudie kosa tena.

Kumfanyia mtoto ukatili kama vile kumchoma, kumkata, kumkanyagakanyaga, kumnyima chakula n.k. Humfanya akue katika hali ya kuwa mkatili au mwenye utu wa ndani ulioathirika.

11. Kumfanyia mtoto kila kitu

Wazazi wengi hufanya kosa la kumfanyia mtoto kila kitu kwa kuamini kuwa ndiko kumhudumia vyema. Watoto huwekewa wahudumu au waangalizi hata zaidi ya mmoja, ili tu wasipate shida.

Ni muhimu mtoto akajifunza kufanya baadhi ya vitu hata kama kuna mwangalizi; mtoto ajifunze vitu kama vile kuoga, kufua, kufagia na hata kupanga vitu katika chumba chake. Kwa njia hii utalea mtoto anayewajibika.

12. Kutokumfundisha mtoto kujiandaa kwa baadaye

Ni lazima mtoto afahamu kwanini anatakiwa kusoma, kulinda afya yake, kutumia pesa vizuri n.k. Wazazi wengi wanafikiri kuwa watoto watajua tu mambo haya wenyewe moja kwa moja siku za mbeleni.

Hili ni kosa ambalo huwafanya watoto wa wazazi wengi hasa wenye pesa kutokuandaa baadaye zao. Wao hufikiri wamezaliwa kutunzwa na baba na mama hadi mwisho wa maisha yao.

13. Kutokutawala ulaji wa mtoto

Ni jambo la kusikitisha kuona mtoto anapata maradhi ya shinikizo la damu kutokana na ulaji mbaya. Wazazi wengi wenye pesa huwapa watoto wao mlo bora kupita kiasi, jambo ambalo huathiri afya za watoto.

Pia wazazi wengine huwazoesha watoto wao vitu kama vile biskuti na pipi ili kuwafurahisha. Jambo hili limewasababishia watoto wengi kuoza meno au hata kuwa wezi wa fedha ili wanunue vitu hivyo.

14. Kutokumfundisha mtoto elimu ya jinsia

Swala la jinsia lipo na haliepukiki; mtu anayeweza kufahamu vyema maswala ya kijinsia ya mtoto ni mzazi. Watoto wengi hufundishwa elimu ya jinsia na marafiki zao shuleni, jambo linalowafanya wapate elimu potofu.

Hivyo ukiwa kama mzazi unayejali baadaye ya mtoto wako, ni vyema ukatenga muda ukazungumza naye kuhusu maswala ya kijinsia.

15. Kutokuheshimu hisia na utu wake

Mtoto ni binadamu kamili mwenye utu na hisia ambavyo vyote vinatakiwa kuheshimiwa. Wazazi wengi hufanya kosa la kutokujali kuwa watoto wao wamechoka, hawana furaha au hata kujali wanapokuwa na changamoto mbalimbali.

Ni muhimu pia wazazi waepuke kuwakaripia au kuwakemea watoto wao mbele ya watoto wengine, kwani kwa kufanya hivyo huwafanya wajisikie duni.

Hitimisho

Naamini umeona wazi jinsi suala la malezi lilivyo pana na gumu. Lakini naamini kwa kuepuka makosa tajwa hapo juu, moja kwa moja wewe kama mzazi utaweza kumlea mtoto wako vyema.

Hakikisha unahusisha imani na juhudi zako zote katika malezi, kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

Je una swali au maoni kutokana na makala hii? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha usisahau kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi. Unaweza pia kuwashirikisha wengine makala hii.

3.3 6 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

14 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
john
john
4 years ago

naomba kujua ni miaka mingapi unatakiwa kulala nao pamoja watoto wako,kwani wazazi hatujui miaka mingapi unatakiwa kulala nao

john
john
4 years ago

ujumbe mzuri sana ,tunaomba mada nyingine

Mariki
Mariki
3 years ago

safi sana

Daniel
Daniel
2 years ago

kazi nzuri

Minah
Minah
1 year ago

Wow somo zuri sana

JACKSON JASTIN MPONGO
JACKSON JASTIN MPONGO
10 months ago

Mungu akubariki sana ndugu sijui makala zako ntazipataje ndugu kiukweli umeelimisha vya kutosha

Thom
Thom
10 months ago

Sawa www

Aretas Silayo
Aretas Silayo
10 months ago

Nahitaji kujua namna ya kulea watoto katika perspective ya kiimani ya Kikristo.

14
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x