Vitu 10 Ambavyo Kila Mzazi au Mlezi Anatakiwa Kumfundisha Mtoto Wake - Fahamu Hili
Thursday, February 22Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Vitu 10 Ambavyo Kila Mzazi au Mlezi Anatakiwa Kumfundisha Mtoto Wake

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Mtoto

Mzazi au mlezi ndiye mwalimu namba moja wa mtoto wake. Kwa kiasi kikubwa sana mtoto hujifunza na kuiga vitu au mambo mbalimbali kutoka kwa wazazi au walezi wake.

Hivyo ni muhimu sana mzazi kuhakikisha anamfundisha mtoto wake mambo muhimu anayopaswa kujifunza ili akue katika malezi bora na awe na baadaye (future) njema.

Kwa kutambua umuhimu wa mzazi au mlezi kumfundisha mtoto wake mambo kadhaa muhimu; karibu ufahamu vitu au mambo 10 ambayo kila mzazi au mlezi anatakiwa kumfundisha mtoto wake.

1. Matumizi mazuri ya muda

Matumizi ya muda ni swala muhimu kwa kila mtu, tena ni msingi wa mafanikio kwa kila mtu. Hivyo mzazi au mlezi anapaswa kumfundisha mtoto wake matumizi ya muda tangu akiwa mtoto ili akue akiwa na tabia hiyo.

Mzazi au mlezi anapaswa kumfundisha mtoto wake maswala kama vile kuamka mapema, kulala kwa wakati, kuwahi eneo husika kwa muda stahiki, kujiwekea ratiba na kuifuata, n.k.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda

2. Matumizi Mazuri ya pesa

Ni watu wachache sana ndiyo wenye matumizi mazuri ya pesa; hii inatokana na kutokujifunza kutumia pesa vyema tangu utoto wao.

Kila mzazi au mlezi anapaswa kumfundisha mtoto wake umuhimu na njia za kutumia pesa vyema.

Ni muhimu mtoto afundishwe kuweka akiba, afundishwe kununua vitu vya maana na si vitu kama pipi na biskuti, afundishwe kutumia pesa kulingana na jukumu la pesa hizo, n.k.

Kumfundisha mtoto tabia hii kutamfanya akue huku akiwa na tabia ya kutumia pesa vyema.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema

3. Elimu ya jinsia

Wazazi au walezi wengi hufikiri kuwa kuwafundisha watoto wao elimu ya jinsia ni kinyume na maadili au ni kuwafundisha tabia mbaya. Hili limetoa mwanya kwa watoto wao kupata elimu potofu kutoka kwa marafiki au watu wasio sahihi.

Ili kumwepushia mtoto mimba za utotoni, ndoa za utotoni au hata magonjwa ya zinaa ni muhimu afundishwe elimu ya jinsia na mzazi au mlezi wake.

4. Tabia ya kusoma vitabu

Vitabu ni chanzo cha maarifa ambacho hakiwezi kubadiliwa na kitu kingine chochote; hata maarifa mengi yaliyoko kwenye mtandao wa intaneti kwa kiasi kikubwa yamechukuliwa kwenye vitabu.

Kila mzazi au mlezi anapaswa kusoma vitabu na kumfundisha mtoto wake tabia ya kusoma vitabu ili ajipatie maarifa mbalimbali yatakayoboresha maisha yake.

Soma pia: Faida 15 za Kusoma Vitabu Unazotakiwa Kuzifahamu

5. Kumwamini Mungu

Kila binadamu ameumbwa awe na imani fulani. Imani humsaidia binadamu kwa njia mbalimbali kamavile kutawala mwenendo au tabia yake pamoja na kumpa tumaini maishani hasa wakati wa uhitaji.

Mtoto aliyefundishwa kumwamini Mungu, na akaliweka swala hilo kwenye matendo ni lazima atakuwa ni mtoto mwenye maadili mema na mafanikio lukuki.

Hivyo kila mzazi au mlezi anapaswa kuwa mfano mwema wa kumwamini Mungu, kumfundisha na kumhimiza mtoto kumwamini Mungu.

Soma pia: Makosa 15 ya Kuepuka Katika Malezi ya Watoto

6. Kujali afya yake

Afya ni swala muhimu kwa kila binadamu, hivyo mzazi au mlezi anatakiwa kumfundisha mtoto wake kujali afya yake.

Mzazi anapaswa amfundishe mtoto kuoga, kufua nguo zake, kunywa maji safi na salama, au hata kuchukua tahadhari nyingine ili kulinda afya yake.

7. Kupenda na kuishi na watu wengine

Mtoto anapaswa kufundishwa upendo na jinsi ya kuishi na watu vyema tokea akiwa mdogo. Mtoto anapaswa kufundishwa kuheshimu na kuthamini watu wengine hata kama siyo wa familia yake.

Swala hili litamfanya mtoto akue katika hali ya kuthamini na kuthaminika kwa wanajamii wote.

8. Kutunza mazingira

Mazingira yanapaswa kutunzwa ili yatunze pia vizazi vijavyo. Hivyo kumfundisha mtoto utunzaji wa mazingira ni kumwezesha kuandaa mazingira bora kwa kizazi chake na cha baadaye.

Mtoto anatakiwa kufundishwa kupanda miti, kutokutupa taka hovyo pamoja na kujali viumbe hai.

9. Sheria na matumizi sahihi ya barabara

Haizuiliki kuwa mtoto ni lazima atatumia barabara katika maisha yake. Ili kuepusha mtoto wako kuwa chanzo cha ajali au yeye mwenyewe kupata ajali, ni muhimu kumfundisha sheria na matumizi sahihi ya barabara.

Ni lazima mtoto afahamu namna salama ya kuvuka barabara pamoja na alama za msingi za barabarani.

10. Kupika pamoja na kazi ndogondogo

Niliandika kupika bila kuijumuisha na kazi zingine kutokana na umuhimu wake. Mtoto anapaswa kufundishwa kuandaa chakula au vinywaji rahisi ili aweze kujihudumia iwapo mzazi hatokuwa karibu.

Kila mtu anafahamu kuwa wasaidizi wa nyumbani wamekuwa ni taabu kupatikana, hata wakipatikana hawawi waaminifu. Hivyo mtoto akifahamu kupika atajihudumia yeye na familia kwa ujumla.

Siyo kupika tu, bali mtoto anapaswa kufundishwa kazi nyingine ndogondogo kama vile kufagia, kudeki, kushona vifungo vya nguo zake, kutunza bustani au wanyama, n.k.

Soma pia: Sababu 7 za Kwanini Kila Mwanaume Anatakiwa Kujua kupika

Hitimisho

Kwa mtu mwenye jicho la kuona naamini ameona vitu vilivyoelezwa hapa jinsi vilivyo muhimu kwenye ukuaji na maendeleo ya sasa na ya baadaye ya mtoto.

Bila shaka upo wajibu ambao mzazi au mlezi kama mwalimu wa karibu anapaswa kuutimiza ili kuhakikisha mtoto wake anakuwa na kufikia malengo yake.

Je wewe huwa unamfundisha mtoto wako vitu hivi? Je ni kipi zaidi unachomfundisha?

5 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Samwel
Samwel
2 years ago

BARIKIWENI SANA

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x