Vitu 10 Ambavyo Wanaume Waliokomaa Hawavifanyi - Fahamu Hili
Wednesday, February 28Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Vitu 10 Ambavyo Wanaume Waliokomaa Hawavifanyi

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Mwanaume

Je mwanaume aliyekomaa ni yupi? Je ni mwenye miaka zaidi ya 18? Kwa kawaida kuna makundi makuu mawili ya wanaume, wanaume wachanga na wanaume waliokomaa.

Kama kulivyo na tofauti kubwa kati ya mtoto mchanga na mtu mzima au aliyekomaa ndivyo ilivyo pia kwa makundi haya mawili ya wanaume.

Mwanaume aliyekomaa ni yule ambaye maamuzi na matendo yake yanahusisha busara, hekima pamoja na utafiti wa kutosha. Ikiwa unapenda kuwa au kumfahamu vyema mwanaume aliyekomaa basi karibu nikufahamishe vitu 10 ambavyo wanaume waliokomaa hawavifanyi.

1. Hawaruhusu hofu kuwazuia kufikia furaha na malengo yao

“Hofu ni mojawapo ya adui mkubwa wa mafanikio.”

Reginald Mengi

Kwa hakika ni kweli kabisa hofu ni adui mkubwa wa mafanikio yetu. Wanaume waliokomaa wanafahamu madhara ya hofu maishani mwao hivyo hawaruhusu hofu hasa ile ya kushindwa iwatawale.

Wanaume hawa hufanya mambo wakiwa na uthubutu wa hali ya juu, wao hawajali walishindwa jana au watashidwa kesho. Hili huwafanya wanaume hawa kufanikiwa sana tofauti na wanaume wachanga.

2. Hawafanyi vitu ili kuwafurahisha wengine

“Siwezi kukupa kanuni ya mafanikio, lakini ninaweza kukupa kanuni ya kushindwa – nayo ni: Jaribu kumridhisha kila mtu.”

Herbert Bayard Swope

Ni wazi kuwa Hubert Bayard Swope alifahamu fika kuwa ukitaka kushidwa jaribu kumfurahisha kila mtu. Wanadamu wanatofautiana, huyu anapenda hiki na huyu kile; hivyo kujaribu kumfurahisha kila mtu ni kujiweka kwenye njia panda ngumu ambayo itakuzuia kufikia malengo yako.

Wanaume waliokomaa hawatafuti kuwafurahisha watu wengine bali wao hupambana kutimiza malengo na maono yao.

3. Matumizi yao hayazidi kipato

Tathimini kubwa ya ukomavu wa mwanaume ni kwa kutazama matumizi yake ya pesa.

Mwanaume mchanga hutumia pesa nyingi kuliko zile anazozipata; kwake vitu kama kununua nguo, simu ya bei, kuhonga wanawake, na pombe ni vitu vya msingi zaidi kuliko kuweka akiba au kuwekeza.

Lakini hali hii ni kinyume kwa wanaume waliokomaa kwani wao huweka akiba, hutumia kidogo kuliko wanachopata tena kwa mambo ya msingi na hufikiri kuhusu kuwekeza.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema

4. Hawayumbishwi na maneno ya wanawake

Umezaliwa peke yako, umekua peke yako, unakuja kuyumbishwa na mtu ukiwa na miaka 18+? Hii si sawa hata kidogo.

Wanaume waliokomaa wanatambua na kuthamini nafasi ya mwanamke kwenye maisha yao, lakini hawaruhusu maneno mabaya ya wanawake yawatishe.

Maneno kama vile “wewe siyo mwanaume mzuri”, “huna hadhi yangu”, “hufai kuwa mume”, “huna hela”, n.k. ni baadhi ya maneno mabaya ya wanawake ambayo mwanaume aliyekomaa haathiriwi nayo.

5. Hawabebi chuki na hasira

Chuki na hasira huathiri afya ya mwili, roho na hata utendaji wako wa kazi. Kubeba chuki hakukusaidii bali kunaendelea kukutesa huku kukimwacha aliyekukwaza akiendelea na maisha yake.

Wanaume waliokomaa huwa na moyo wa kusema acha yapite au yaishe; kisha huendelea na maisha na shughuli zao za kila siku.

Soma pia: Sababu 9 za Kwanini Umsamehe Aliyekukosea

6. Hawajihisi wadhaifu juu ya mwonekano wao

Mwanaume hasifiwi sura bali anasifiwa kwa mafanikio au malengo aliyoyatimiza. Wanaume waliokomaa hawajali kuwa mimi nina sura mbaya au mimi sina mvuto kama wa fulani n.k.

Nikukumbushe pia kuwa masuala kama vile kunyoa kiduku, kuvaa milegezo au kuiga kila mtindo wa mavazi ni maswala ya kivulana tena ya wanaume wachanga ambao hawajakomaa.

Wanaume waliokomaa hutafuta mafanikio halisi, tena ya kudumu na siyo vitu vya nje kama vile sura au mvuto kwa wanawake.

7. Hawakai mbali na familia zao

Ukimwona mwanaume ambaye anakimbia familia yake, huyo bado ni mchanga sana. Fahari ya mwanaume yoyote aliyekomaa ni kuona yuko karibu na anaihudumia familia yake kila mara.

Kama baba yako au mkeo anakutunzia kila kitu cha familia yako sasa kwanini usiitwe mwanaume suruali? Mwanaume aliyekomaa hujali wajibu wake na kuhakikisha anakaa katika nafasi yake kama baba wa familia.

8. Hawaingii kwenye mahusiano yasiyo na lengo

Ukiona mwanaume ambaye kila msichana anayepita mbele yake anataka kuwa naye kwenye mahusiano, basi mtafutie chupa ya maziwa kwa sababu bado ni mchanga sana.

Mahusiano siyo kama daladala upande na kushuka, mahusiano ni kitu kinachotakiwa kufanywa kwa malengo na kwa ubora stahiki.

Wanaume waliokomaa huingia kwenye mahusiano ya maana tena yenye lengo la maana kama vile ndoa na si vinginevyo.

9. Hawachukii kazi zao

Unamkuta mtu kila saa analalamika hii kazi, hii kazi, hii kazi naichukia, hii kazi inanitesa, hii kazi siyo ya hadhi yangu, n.k. Lakini bado unamwona hapo anamaliza soli kuifuata na kuifanya kila siku.

Wanaume waliokomaa huthamini na kupenda kazi zao hata kama ni mbaya; wanatambua fika kuwa ubaya wa kitu unazidi kutokana na hisia ulizo nazo moyoni.

Kulalamika na kulaumu juu ya kazi ni tabia ya wanaume wachanga; ikiwa kazi inakushinda basi iache utafute nyingine au ujiajiri kama unaweza kuliko kuendelea kulalama.

Soma pia: Maswali 10 Muhimu ya Kujiuliza Kabla ya Kuacha Kazi

10. Hawaogopi kuchukua maamuzi magumu

Kuna wakati kwenye maisha mtu unahitajika kufanya maamuzi magumu juu ya maswala mbalimbali. Wanaume waliokomaa huwa na uthubutu mkubwa tena bila hofu wa kufanya maamuzi magumu ambayo yatawanufaisha sasa na baadaye.

Hapa ninamkumbuka mtu mmoja aliyenieleza jinsi alivyochukua ujasiri mkubwa wa kuvunja mahusiano ya miaka minne na mpenzi wake baada ya mpenzi wake kuanza tabia ambazo zingegharimu ndoa yao iliyokuwa ifungwe karibuni.

Nakumbuka maneno aliyoniambia, alisema “Gharama ya kuvunja ndoa ni kubwa kuliko gharama ya kuvunja uchumba. Hivyo nimeamua kuachana na huyu mchumba wangu.”

Nampongeza sana kwani sasa ameshapata mwenzi murwa wa maisha na wamejaliwa watoto wawili huku yule mpenzi wake wa awali akihangaika mitaani bila tumaini.

Hii linatupa funzo kuwa mwanaume aliyekomaa anapaswa kuwa na uthubutu wa kuchukua maamuzi magumu, si tu katika mahusiano bali katika maswala yote yanayogusa maisha yake.

Soma pia: Sifa 17 za Kuzingatia Kwa Mtu Unayetaka Kuoa au Kuolewa Naye

Hitimisho

Natumaini sasa umejifunza na umeona wazi tofauti iliyopo kati ya mwanaume mchanga na aliyekomaa kwa kupitia vitu hivi ambavyo wanaume waliokomaa hawavifanyi.

Je wewe uko katika kundi gani? Ikiwa uko kwenye kundi la wanaume waliokomaa, je wewe huwa hufanyi nini zaidi ya vitu hivi 10?

Tafadhali andika maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

4.5 2 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

6 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Edwin mashimba
Edwin mashimba
4 years ago

Kuchukua maamuzi magumu

Ozem
Ozem
3 years ago

Ninajifunza sana , na ninawashukuru kwa makala hizi

Christophe
Christophe
1 year ago

Inafurahisha na kuleta mwangaza sana,

6
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x