Faida 10 za Kusoma Nje ya Nchi - Fahamu Hili
Saturday, April 20Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Faida 10 za Kusoma Nje ya Nchi

Washirikishe Wengine Makala Hii:
Nje ya Nchi
Chanzo cha picha: https://blog.studocu.com

Watu wengi wamekuwa wakitamani kusoma nje ya nchi, labda ni kutokana na kupata safari nyingi za ndege au fedha za udhamini wa masomo.

Kwa hakika kusoma nje ya nchi kuna manufaa makubwa sana zaidi ya kusafiri kwa ndege pamoja na kupata fedha za udhamini wa masomo.

Ikiwa unataka kuongeza maarifa au unataka kusoma nje ya nchi, basi fahamu faida 10 za kusoma nje ya nchi.

1. Kuongeza uwezo wako wa lugha

Kusoma kwenye nchi nyingine itakulazimu kujifunza lugha ya nchi husika ili uweze kuwasiliana na kuitumia kujifunza mambo mbalimbali.

Kwa mfano watu wengi wanaosoma nchi za ulaya huongeza uwezo wao wa kuzungumza kiingereza zaidi.

Hivyo kusoma nchi za kigeni kutakuwezesha kujifunza na kuongeza uwezo wako wa lugha za kigeni kama vile Kichina, Kifaransa, Kijapani, Kiingereza, Kijerumani, n.k.

Soma pia: Mbinu 10 za Uhakika za Kufahamu Kiingereza/English kwa Muda Mfupi

2. Kujifunza utamaduni mpya

Kila nchi ina utamaduni wake ambao kwa namna moja au nyingine unatofautiana na wa nchi nyingine. Unapokwenda kusoma nje ya nchi, ni wazi kuwa utajifunza utamaduni mwingine tofauti na ule uliouzoea.

3. Kupata marafiki

Marafiki ni muhimu sana kwenye maisha, hasa marafiki sahihi. Kwa njia ya kusoma nje ya nchi utajipatia marafiki toka sehemu mbalimbali duniani; hii ni kutokana na kukutana na watu kutoka nchi mbalimbali mara uwapo chuoni.

Marafiki hawa utakaowapata kutokana na kusoma nje ya nchi wanaweza kukufaa kwenye maisha yako yote. Inawezekana pia ukapata mwenzi wa maisha unaposoma nje ya nchi.

4. Kujifunza mfumo mpya wa elimu

Mifumo ya elimu hutofautiana kati ya taifa moja na jingine. Hivyo kusoma nje ya nchi kutakuwezesha kuufahamu vyema mfumo wa elimu wa nchi nyingine. Kwa njiaa hii utaongeza maarifa na ujuzi wako zaidi.

5. Kupanua uwezo wako wa kufikiri

Watu wengi wanaposoma nje ya nchi, hujikuta wakipata fikra pana na uzoefu mkubwa kutokana na yale waliyoyaona huko nje.

Nimeshuhudia watu wakirudi kwenye nchi zao na kutekeleza miradi mikubwa ya kushangaza kutokana na mawazo na fikra chanya walizozipata walipokuwa wanasoma nje ya nchi.

6. Kuufahamu ulimwengu

“Kutembea ni kuona mengi.”

Unaposafiri kwenda nchi nyingine kwa ajili ya masomo, ni wazi kuwa utajifunza na kuufahamu ulimwengu zaidi.

Uwapo masomoni unaweza kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi husika na ukajifunza mambo mbalimbali tofauti na kusoma ndani ya nchi yako.

7. Kuongeza soko lako la ajira

Baadhi ya kampuni au taasisi hupendelea kuajiri watu waliosoma nje ya nchi kwa kuamini kuwa wamepata elimu bora zaidi.

Hili linaweza kushuhudiwa kwenye nafasi za kazi kwenye makapuni ya kigeni au ofisi za balozi mbalimbali, kwani huajiri zaidi wale waliosoma nje ya nchi.

Ni mara chache sana watu waliosoma nje ya nchi na kufaulu vizuri wakakosa ajira.

8. Hukutengenezea kumbukumbu isiyosahaulika

Unaposoma nje ya nchi unajipatia kumbukumbu muhimu isiyoweza kufutika kirahisi. Ni wazi kuwa utakumbuka ulivyoacha ndugu na familia, changamoto ulizokumbana nazo ugenini pamoja na mambo mbalimbali yaliyokuvutia ulipokuwa masomoni.

9. Huongeza uzoefu wa maisha

Unapokuwa nje ya nchi kwa ajili ya masomo utajifunza mengi na kufanya mengi; utatakiwa kujipangia ratiba, kutumia pesa vyema, kujihudumia, n.k.

Hivi vitakupa uzoefu mkubwa wa maisha jambo ambalo ni tofauti na kukaa kwenye familia yako ndani ya nchi yako.

Soma pia: Tabia 10 zitakazobadili maisha yako

10. Hukuwezesha kuthamini vitu

Mara nyingi huwezi kuthamini kitu hadi pale unapokikosa. Unapokuwa nje ya nchi utakosa ndugu uliowazoea, vyakula, nguo, maeneo, au hata vitu vingine unavyovipata kwenye nchi yako.

Hili litakuwezesha kuthamini vitu na kujifunza kutumia vyema vile vitu vichache utakavyokuwa navyo nje ya nchi.

Hitimisho

Naamini umefahamu bayana kuwa kuna manufaa mengi sana ya kusoma nje ya nchi kuliko kupanda ndege pamoja na kupata udhamini wa masomo.

Ikiwa umepata neema ya kusoma nje ya nchi, basi usiache bali itumie vizuri ili uweze kupata faida zilizojadiliwa katika makala hii.

Soma pia: Mambo 17 ya Kuzingatia Kabla ya Kusafiri Kwenda Nchi Nyingine

Je una maoni yoyote? Tafadhali tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

4 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x