Mambo 10 ya Kuzingatia Unapomtafutia Mtoto Shule - Fahamu Hili
Thursday, February 22Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kuzingatia Unapomtafutia Mtoto Shule

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Wanafunzi

Hivi leo kuna shule nyingi, lakini siyo shule zote ni bora au zinafaa kwa ajili ya mtoto wako. Hii ni kutokana na shule nyingi kuanzishwa na kuendeshwa kwa misingi ya kibiashara kuliko huduma.

Swala la kuhakikisha mtoto wako anapata elimu bora ni swala la msingi. Hii ni kutokana na nafasi na umuhimu wa elimu kwa maisha ya sasa na ya baadaye ya mtoto.

Ikiwa unataka kupata shule nzuri kwa ajili ya mtoto wako, karibu nikufahamishe mambo 10 ya kuzingatia unapomtafutia au kumchagulia mtoto wako shule.

1. Kiwango cha ufaulu

Hakuna mzazi au mlezi ambaye anapenda mtoto wake asifanikiwe kwenye masomo. Kufanikiwa kwa mtoto kwa kiasi kikubwa kunategemea kiwango cha ufaulu cha shule.

Ni wazi kuwa shule inayofaulisha vyema itakuwa inafundisha vyema pia. Hivyo kagua kwanza matokeo ya mitihani, hasa ya kitaifa ya shule unayotaka kumpeleka mwanao.

2. Upatikanaji wa huduma na usalama

Baadhi ya shule hazina huduma muhimu wala usalama wa kutosha. Kumeshuhudiwa baadhi ya shule zikivamiwa na vibaka au hata wanafunzi wakihangaika siku nzima kutafuta huduma kama vile maji.

Ni muhimu kuhakikisha usalama na huduma kama vile maji na umeme vinapatikana vyema kwenye shule husika ili mwanao apate utulivu na muda wa kutosha wa kujikita kwenye masomo.

3. Huduma za kiafya

Mwanao awapo shuleni atahitaji uangalizi na huduma za kiafya. Baadhi ya shule hazina huduma nzuri za afya au utaratibu wa kuwahudumia wanafunzi.

Nimeshuhudia kwenye baadhi ya shule wanafunzi wakiugua hata kukaribia kufa kutokana na kutokuwepo kwa huduma au utaratibu wa kutunza afya za wanafunzi.

Hivyo kabla ya kumpeleka mwanao kwenye shule fulani hakikisha ina huduma nzuri za afya kwa ajili ya wanafunzi wake.

4. Nidhamu

Nidhamu ni msingi wa mafanikio ya kitaaluma. Baadhi ya shule zina kiwango duni sana cha nidhamu; shule hizi wanafunzi huvuta bangi, hutoroka hovyo, huendesha migomo, n.k.

Kwa hakika ukimpeleka mwanao kwenye shule kama hii hatoweza kufanya vizuri kwenye taaluma.

5. Mazingira ya kujifunzia na waalimu

Mazingira ya kujifunzia pamoja na ubora na kiasi cha waalimu ni muhimu sana katika ufaulu wa mtoto.

Hebu fikiri shule haina waalimu wa kutosha, maabara, madarasa ya kutosha, vitabu, au madawati ya kutosha; je kweli mtoto wako ataweza kujifunza vyema? Kwa hakika hataweza.

Ni muhimu kuhakikisha pia mazingira ya kujifunzia ni rafiki, kwa mfano shule za katikati ya mji siyo nzuri kwani zina usumbufu mwingi.

6. Gharama za ada

Kila mzazi ana mfuko wake wa pesa, vivyo hivyo kila shule ina gharama zake. Hakikisha unamudu gharama za ada za shule husika kabla ya kumpeleka mwanao.

Shule nyingi huwarudisha nyumbani aua hata kuwasimamisha kuendelea na masomo wanafunzi wale walioshindwa kukamilisha ada. Swala hili si zuri kwani linaweza kuathiri kiwango cha taaluma cha mtoto.

7. Eneo shule ilipo

Baadhi ya shule zipo maeneo mabaya ambayo hayafikiki kwa urahisi. Hakikisha unaweza kufika wewe au mwanao katika shule unayotaka kuichagua bila shida.

Hili litasaidia pale ambapo mzazi au mlezi atahitajika shuleni au wakati wa kumwona mtoto apatapo shida itakuwa ni rahisi.

8. Idadi ya wanafunzi

Kadri idadi ya wanafunzi inavyozidi kuwa kubwa ndivyo na ubora wa elimu unavyopungua. Hakikisha kama shule unayotaka kuichagua ina wanafunzi wengi, basi iwe inawamudu vyema.

La sivyo chagua shule ambayo ina idadi ya wanafunzi ya wastani ambayo haiathiri kiwango na ubora wa elimu inayotolewa.

9. Mafunzo na shughuli za ziada

Baadhi ya shule hutoa mafunzo na shughuli za ziada kama vile mafunzo ya kompyuta, lugha za kigeni au hata shughuli kama vile kilimo na michezo.

Kumpeleka mtoto wako katika shule za aina hii kutamuwezesha kujifunza vitu vya ziada tofauti na vile anavyojifunza darasani.

Kwa njia hii utamwandaa kukabiliana na ulimwengu wa ushindani kwenye maisha yake ya baadaye.

10. Ushirikishwaji wa wazazi

Baadhi ya shule wakishampokea mwanao pamoja na pesa, basi mkataba wako umekwisha. Ni muhimu kuchagua shule ambayo inawashirikisha wazazi au walezi katika mipango ya shule na maendeleo ya watoto wao.

Kwa kuchagua shule yenye mahusiano mazuri na mzazi kunafanya ufuatiliaji wa maendeleo ya mtoto uwe rahisi. Kumbuka! Ufuatiliaji wa maendeleo ya mtoto ni muhimu ili uweze kubaini na kushughulikia mambo ambayo hayaendi vizuri.

Hitimisho

Kwa kuzingatia makala hii naamini sasa hutompeleka tena mwanao kwenye shule yoyote bali utahakikisha unampeleka kwenye shule bora.

Elimu bora ni muhimu sana kwa ajili ya maandalizi ya baadaye ya mtoto wako, hivyo hakikisha unazingatia mambo tajwa kwenye makala hii wakati unapomtafutia mtoto wako shule.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini. Karibu uwashirikishe wengine makala hii pamoja na kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x