Changamoto 12 za Ujasiriamali na Jinsi ya Kuzikabili - Fahamu Hili
Thursday, February 22Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Changamoto 12 za Ujasiriamali na Jinsi ya Kuzikabili

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Gengeni

Kila jambo lina changamoto zake, ujasiriamali nao unachangamoto zake nyingi. Ni wazi kuwa wajasiriamali wakubwa na wadogo, wote hukutana na changamoto; tofauti yao ni chanzo cha changamoto hizo na njia wanazozitumia kuzikabili.

Wajasiriamali wadogo ndiyo wamekuwa wakikabiliwa zaidi na changamoto hizo na hata kupelekea kupoteza biashara au miradi yao.

Inawezekana wewe ni mmoja wapo wa wajasiriamali wanaokabiliana na changamoto. Karibu nikushirikishe changamoto 12 za ujasiriamali na jinsi ya kuzikabili.

1. Mtaji

Kila biashara inahitaji mtaji ili iweze kujiendesha na kujipanua. Wajasiriamali wengi wanashindwa kuanzisha biashara au kupanua biashara zao kutokana na kukosa mtaji.

Suluhisho:

Kumbuka! Siyo lazima upate mtaji wote unaouhitaji, unaweza kuanza na mtaji kidogo sana na ukaukuza taratibu.

Zipo njia nyingi sana za kupata mtaji kwa ajili ya biashara au umradi wako. Unaweza kutumia njia zifuatazo:

 • Uza baadhi ya vitu vyako ambavyo si vya lazima sana. Kwa mfano ikiwa una simu ya bei kubwa, mikoba, nguo au vifaa vya kielektroniki kama vile TV na Subwoofer ambavyo huvitumii sana, unaweza kuviuza na ukapata mtaji wa kuanzisha biashara yako.
 • Azima au omba pesa kwa rafiki au ndugu anayekuamini. Ikiwa una ndugu au rafiki anayekuamini unaweza kumwomba akupe kiasi fulani cha pesa na utamrudishia utakapopata faida.
 • Jiunge na vikundi vya wajasiriamali. Vipo vikundi mbalimbali vinavyowawezesha wajasiriamali hasa wadogo kupata mitaji. Hakikisha kikundi unachojiunga nacho kinaaminika na kina masharti unayoweza kuyafuata.
 • Kopa pesa kutoka kwenye taasisi za kifedha. Njia hii nimeiweka mwishoni kwakuwa mara nyingi haifai sana kwa wajasiriamali wanaoanza. Ikiwa biashara yako au mradi wako umeshakuwa kwa kiasi fulani, unaweza kukopa pesa kwenye tasisi hizi na ukaongeza mtaji wako.

Soma pia: Jinsi ya Kuanza Biashara na Mtaji Mdogo.

2. Ushindani

Biashara au mradi mingi ya wajasiriamali ina ushindani mkubwa kutokana na kufanywa na watu wengi. Hata hivyo bado wewe kama mjasiriamali unaweza kukabili changamoto ya ushindani.

Suluhisho:

Unaweza kukabili changamoto ya ushindani kwa kufanya haya yafuatayo.

 • Uza bidhaa inayoendana na muda wa sasa. Kwa mfano kama unauza redio, tambua kuwa watu hawanunui redio zinazotumia kanda tena, bali wanataka redio zinazotumia USB pamoja na CD. Kwa kuzaa vitu kuendana na wakati utaweza kukabili ushindani vyema.
 • Uza kwa punguzo au bei ya chini kidogo tofauti na wengine.
 • Lenga matatizo ya watu katika bidhaa na huduma yako. Watu wananunua bidhaa kwasababu wanataka zitatue matatizo yao na si vinginevyo.
 • Jitangaze jinsi ipasavyo. Watu hawatanunua bidhaa yako kama hawakufahamu, hivyo hakikisha unajitangaza kwa wateja.

Soma pia: Mbinu 10 za Kuongeza au Kuvutia Wateja Kwenye Biashara.

3. Mzunguko wa pesa

Inawezekana una mtaji mzuri lakini mzunguko wa pesa unakuwa mgumu katika biashara yako. Hili linaweza kusababishwa na maswala kama vile watu au taasisi zinazodaiwa na biashara yako kuchelewa kulipa madeni yao kwa wakati.

Changamoto inatokea pale ambapo wewe unataka kulipa wale wanaokupa huduma na bidhaa mbalimbali lakini unakuwa bado hujapata pesa kutoka kwa wadaiwa wako.

Suluhisho:

Unaweza kutumia njia zifuatazo kukabili changamoto ya mzunguko wa pesa.

 • Weka bajeti nzuri kwenye biashara au mradi wako. Kuweka bajeti nzuri kutakuwezesha kuwa na pesa za akiba ambazo zitakusaidia kuendesha biashara wakati utakapokuwa na mzunguko duni wa pesa.
 • Fuatilia na kumbusha malipo yaliyoko nje. Ikiwa kuna watu au taasisi ambazo unazidai, basi wakumbushe na ufuatilie pesa hizo ili ziweze kulipwa na kukidhi mahitaji ya biashara yako.
 • Punguza matumizi yasiyo ya lazima. Unapokuwa kwenye changamoto ya mzunguko duni wa pesa, inakupasa kupunguza matumizi yote yasiyo ya lazima ili upate pesa kwa ajili ya mambo ya lazima.

4. Kuchagua bidhaa ya kuuza au wazo la kibiashara

Wajasiriamali wengi hasa wale wanaoanza, hushindwa kujua ni bidhaa gani wanayoweza kuuza au ni wazo gani la kibiashara wanaloweza kulitekeleza.

Hili huwafanya kushika hiki na kile na kuacha au kufanya vitu wasivyovipenda wala kuvimudu.

Suluhisho:

Unaweza kuzingatia haya yafuatayo wakati wa kuchagua bidhaa ya kuuza au wazo la kibiashara.

 • Chagua wazo au bidhaa unayoipenda na kuimudu kuifanyia kazi.
 • Angalia wakati na uhitaji wa bidhaa husika.
 • Angalia upatikanaji wa mtaji. Hakikisha unaweza kupata angalau mtaji mdogo wa kuanzia biashara unayotaka kuichagua.

Soma pia: Mambo 5 ya Kuzingatia Kabla ya Kuchagua Wazo la Biashara.

5. Masoko

Hauwezi kupata faida na kukuza biashara au mradi wako kama hutouza bidhaa zako.

Kutokana na uelewa duni wajasiriamali wengi hawajui kutafuta wala kuandaa mikakati ya kupata masoko. Hili linakuwa ni changamoto kwao kwani bidhaa zao haziuziki.

Suluhisho:

Unaweza kufanya haya yafuatayo ili kukabili changamoto ya masoko.

 • Tafuta mtaalamu wa masoko akusaidie na kukushauri jinsi ya kupata masoko ya bidhaa yako. Siyo lazima utumie watu wanaolipwa pesa nyingi, bali unaweza kumtafuta rafiki au mtu wa karibu mwenye taaluma ya masoko akakusaidia.
 • Hakikisha unafahu soko na uhitaji kabla ya kutengeneza bidhaa. Hili litakusaidia kutengeneza bidhaa ambazo zinahitajika sokoni.

6. Ukosefu wa elimu

Wajasiriamali wengi wanakwama kwenye shughuli zao kutokana na kukosa elimu stahiki ya ujasiriamali. Wengi hawafahamu usimamizi wa miradi, pesa au hata biashara.

Ikizingatiwa nchi nyingi za Kiafrika bado hazijaandaa mtaala au mfumo mzuri wa kuwafundisha wajasiriamali. Hili linakuwa ni changamoto kubwa kwani hata yale mafunzo machache yanayopatikana hutolewa mijini tena kwa gharama kubwa.

Suluhisho:

Ili kukabili changamoto hii ya elimu au maarifa ya ujasiriamali unaweza kufanya haya yafuatayo.

 • Tumia maarifa kutoka kwenye mtandao. Badala ya kutumia simu au kompyuta yako kwenye mitandao ya kijamii, unaweza kutembelea mamia ya tovuti zinazotoa mafunzo mbalimbali juu ya ujasiriamali. Tovuti yetu ya Fahamuhili.com ni mfano mmoja wapo wa tovuti hizo. Hakikisha unatafuta tovuti sahihi yenye ubora.
 • Jiunge na wajasiriamali wengine kisha mumuite mtu aje kuwafundisha. Kuita mwalimu wa ujasiriamali kama kikundi ni rahisi zaidi kuliko kumwita kama mtu binafsi.
 • Hudhuria semina za ujasiriamali. Inawezekana unaogopa gharama au umbali, lakini kumbuka hii ni njia nyingine nzuri ya kukupa maarifa.

7. Sera duni za kiserekali

Serekali zetu za kiafrika bado zina sera duni ambazo siyo rafiki kwa wajasiriamali.

Wajasiriamali hukutana na milolongo mirefu ya kupata vibali na nyaraka muhimu au kukabiliwa na mizigo mikubwa ya kodi. Hili huwakatisha tamaa na kuwakwamisha wajasiriamali wengi.

Suluhisho:

Kwa hakika suluhisho kubwa na la kudumu ni serikali zetu kutengeneza mazingira na sera rafiki kwa wajasiriamali. Hata hivyo kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya.

 • Anza kidogo kidogo. Unapoanza na vitu vingi au mradi mkubwa mwanzoni, ni wazi sera na kanuni mbovu vitakukabili moja kwa moja.
 • Uliza waliokutangulia walifanyaje kukabili mazingira magumu yanayokukwamisha.
 • Epuka njia za mkato. Kamwe usianze mradi kwa mambo kama vile kukwepa kodi au kwa kutumia vibali bandia, kwani utakapobainika utafilisiwa au hata kushitakiwa. Anza taratibu nawe utapata upenyo hata kama hali ni ngumu.

8. Kuajiri

Kuna wakati wewe kama mjasiriamali unahitaji kuajiri mtu ili akusaidie kutimiza jukumu fulani. Wajasiriamali wengi wanajikuta wakiajiri watu ambao hawafai au wasioweza kuwamudu. Hivyo hili huwa ni changamoto kubwa kwa baadhi ya wajasiriamali.

Suluhisho:

Unaweza kufanya mambo yafuatayo kabla ili kukabili changamoto hii.

 • Tathimini kama ni wakati sahihi. Kuna wakati sahihi ambapo kweli unahitaji mtu mwingine; hakikisha unaajiri mtu unayemhitaji.
 • Ajiri mtu mwenye sifa stahiki. Usiajiri mtu kwa kuwa ni rafiki, ndugu au mpenzi wako; bali hakikisha mtu unayemwajiri ataweza kutekeleza majukumu yake vyema na kuiletea biashara yako faida.

9. Matumizi ya muda

Kuna mtu mmoja aliwahi kusema ukitaka kuoa usioe au kuolewa na mjasiriamali kwani hana muda. Ni kweli wajasiriamali wengi huzidiwa sana kiasi cha kukosa muda wa maswala yao binafsi.

Suluhisho:

Kuna mikakati kadhaa unayoweza kuifanya wewe kama mjasiriamali ili kukabili changamoto ya muda.

 • Panga ratiba na uifuate.
 • Ondoa mambo yasiyo ya lazima kwenye ratiba yako.
 • Gawa majukumu. Kubeba majukumu yote wewe mwenye kunakufanya uzidiwe na ukose ufanisi.
 • Weka malengo na uyafuate.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda.

10. Kupanga majukumu

Hii ni changamoto inayowakabili wajasiriamali wengi, kwani wanashindwa kupanga majuku yao vyema; hawajui wampe nani jukumu lipi na lipi wafanye wao. Hili huwafanya kufanya kila kitu na hatimaye kuharibu zaidi.

Suluhisho:

Unaweza kutumia njia zifuatazo kukabili changamoto hii.

 • Andaa mwongozo wa kufanya kila kazi. Huu utawawezesha wale unaowagawia majukumu kufanya kazi vyema.
 • Panga majukumu kwa watu stahiki.
 • Kagua kila kazi ili kuhakikisha imefanywa vyema na mtu husika.
 • Toa ushauri na mapendekezo pale ambapo utendaji haukuwa sawa.

11. Kuacha kazi ya awali

Changamoto hii huwakabili wajasiriamali wale wanaotaka kuacha kazi yao ya awali ili wawe wajasiriamali. Maswali mengi huibuka akilini mwao kama vile je nitapata faida? Nianzeje? Nani atanisaidia? Nitafanya nini? Nikishindwa itakuaje? Na  mengine mengi.

Suluhisho:

Hakuna kitu kinachoshinda nia na mipango stahiki. Usiogope kuwa mjasiriamali kama tayari una nia na mipango madhubuti.  Kwa mfano kama una akiba ya kutosha na unampango mzuri wa kibiashara, hakuna haja ya kuhofu.

Soma pia: Mambo 7 ya Kufanya Kabla ya Kuanzisha Kampuni au Biashara.

12. Kukata tamaa na kujilaumu

Wajasiriamali wengi hukata tamaa au kujilaumu hasa pale wanapokutana na changamoto zinazotokana na maamuzi au matendo yao.

Suluhisho:

Kumbuka kuwa hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa bila kukutana na changamoto. Jipe moyo usikubali kupoteza sehemu ya kazi ambayo tayari umeshaifanya.

Weka mikakati sahihi, usijilaumu bali jifunze kutokana na kosa ili lisitokee tena wakati mwingine.

Soma pia: Nukuu (Quotes) 50 Zitakazo Kuhamasisha Maishani Mwako.

Hitimisho

Kwa hakika zipo changamoto nyingi za ujasiriamali, lakini kwa hizi kubwa chache nilizozibainisha sambamba na njia za kuzikabili, naamini hutokwama tena.

Je kuna changamoto nyingine inayokukabili? Tafadhali tuandikie maswali au maoni yako hapo chini kuhusu makala hii juu ya changamoto za ujasiriamali.

Usisahau kuwashirikisha wengine makala hii pamoja na kujiunga nasi kwa njia ya barua pepe hapo chini au kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

4.8 4 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

13 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Costantine J. Mauki
Costantine J. Mauki
4 years ago

Hongereni, mpo vizuri!

Costantine J. Mauki
Costantine J. Mauki
4 years ago

Nimeelimika!

benson
benson
Reply to  Kornelio Maanga
3 years ago

ahsante kwa ushauri mzuri ila nina swali mm naitaji kuanzisha biashara kwenye eneo ninaloishi ila tatizo ni kwamba hakuna mzunguko wa biashara je, nifanyeje?

Said Maumba
Said Maumba
3 years ago

ni vizuri sana….Hii itamsaidia mjasiriamali kuweza kufanya vizuri biashara zake.Kiukweli MAFANIKIO=UTATUZI WA CHANGAMOTO.

#Nimeipenda hii

David mura gimugu
David mura gimugu
3 years ago

Asante sana

E. Mashambo
E. Mashambo
10 months ago

Kazi nzuri hongereni

Damas F. Masanja
Damas F. Masanja
8 months ago

Good

13
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x