Makosa 25 ya Kuepuka Unapotengeneza Tovuti (website) au Blog - Fahamu Hili
Saturday, April 20Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Makosa 25 ya Kuepuka Unapotengeneza Tovuti (website) au Blog

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Tovuti

Kuna tovuti na blog nyingi zinazotengenezwa kila siku, lakini siyo zote zinakidhi viwango vya ubora. Hili linasababishwa na tovuti nyingi kutengenezwa bila kuzingatia kanuni muhimu za utengenezaji wa tovuti au blog.

Zipo athari nyingi za kutengeneza tovuti zenye ubora mdogo kama vile kupoteza wasomaji au watembeleaji pamoja na kupata nafasi ndogo kwenye injini pekuzi.

Ni muhimu ukafahamu kuwa  tovuti (website) au blog ni sura yako au ya biashara yako kwenye ulimwengu. Hivyo ikiwa hutozingatia utengenezaji bora wa tovuti au blog yako, basi utaharibu picha yako au ya biashara yako.

Ikiwa unataka kutengeneza tovuti (website) au blog bora, basi fahamu makosa 25 yakuepuka wakati wa kutengeneza tovuti au blog.

1. Muundo mbaya wa tovuti au blog

Kosa la muundo mbaya wa tovuti hufanywa na watu wengi sana, hasa kutokana na maarifa duni ya usanifu mtandao. Kwa mfano unakuta menu iko huku, ukurasa huu uko kule, tangazo limefunika maandishi, vitu vimejibana kwa pembeni n.k. (Mf. https://www.lingscars.com/)

Ni muhimu ukahakikisha tovuti yako inasomeka vizuri na inavutia; ikiwa utatumia kiolezo (template) basi hakikisha unachagua kiolezo kizuri na cha kisasa

2. Mwandiko usiosomeka

mwandiko

Mwandiko unaofaa kwako unaweza usifae kwa wasomaji wako. Hivyo kumbuka uwezo wa kuona na upendeleo wa miandiko hutofautiana baina ya mtu na mtu. Ni muhimu kuhakikisha mwandiko unaoutumia kwenye tovuti au blog yako unasomeka vizuri kwa kila mtu.

3. Kasi ndogo ya kufunguka

Kutokana na usanifu duni, matumizi ya teknolojia ya zamani au hata kuweka mambo mengi kupita kiasi katika ukurasa mmoja, kunafanya tovuti nyingi kuwa na kasi ndogo ya kufunguka. Unaweza kufanya haya yafuatayo:

 • Punguza picha, video au sauti zinazopunguza kasi ya kufunguka.
 • Tumia teknolojia za kisasa zinazowezesha tovuti au blog kufunguka kwa kasi (Web compression and caching).
 • Punguza tovuti za nje zinazofungukia ndani ya tovuti yako kwa njia ya iframe.
 • Tumia webhost bora.

Kama utazingatia mambo haya, utaweza kuongeza watembeleaji zaidi kwani hakuna mtu anayependa kusubiri kusoma tovuti inayochukua muda mrefu kufunguka.

4. Kulazimisha usajili

Kamwe usifanye kosa la kumlazimisha msomaji au mtembeleaji kujisajili kwa lazima. Hakikisha unaandaa maudhui bora au unampa msomaji kitu chenye thamani kwake kitakachomfanya ajisajili mwenyewe.

Hakuna mtu atakayepoteza muda kujisajili kwenye tovuti yako ikiwa anaweza kupata kitu anachokitaka kutoka kwenye tovuti nyingine bila kujisajili; hivyo utapoteza kiasi kikubwa cha watembeleaji.

5. Sauti au video zinazocheza zenyewe

Hakuna kitu ninachokichukia kwenye tovuti kama video au sauti zinazocheza zenyewe. Vitu hivi ni vibaya kwani vinamaliza data pamoja na kutoa maudhui ambayo mtembeleaji hayahitaji.

Mara ninapofungua tovuti na kukutana na vitu hivi, wazo la kwanza linalonijia kichwani ni kufunga tovuti husika; je unafikiri ni mimi peke yangu nitafunga tovuti husika?

Ni wazi kuwa watumiaji wengi wataondoka kwani unawalazimisha kusikiliza au kutazama vitu wasivyovipenda. (Mfano wa tovuti kama hii ni: https://www.lingscars.com/)

6. Matumizi mabaya ya picha

Picha ni sehemu muhimu ya tovuti au blog ikiwa zitatumiwa jinsi ipasavyo. Hakikisha unatumia picha zenye ubora stahiki, tena ambazo hazifunguki kwa tabu.

Epuka kutumia picha kubwa sana au za gif ikiwa hakuna ulazima; unaweza kutumia picha nzuri za ukubwa wa wastani ili usipunguze kasi ya kufunguka kwa tovuti au blog yako.

7. Matangazo yanayokera

Nani asiyependa kupata pesa kupitia blog? Naamini hakuna; ikiwa unapenda kuweka matangazo mbalimbali kwenye tovuti au blog yako hakikisha matangazo husika hayamkeri mtumiaji.

Tumia matangazo machache na mazuri ambayo hayataingilia utendajikazi mzuri wa tovuti au blog yako.

Kumbuka kuepuka matangazo yanayovamia kivinjari (browser) ya mtumiaji na kufanya mambo mbalimbali bila ridhaa yake.

8. Kukosekana kwa fomu ya utafutaji

Hakikisha kama unataka kutengeneza tovuti au blog nzuri, huachi kuweka fomu ya kumuwezesha masomaji kutafuta vitu kwenye tovuti au blog yako.

Hakikisha kila kilichoko kwenye tovuti yako kinaweza kupatikana kupitia fomu ya utafutaji (search field).

Kumbuka ikiwa mtembeleaji atahitaji kufahamu kama kitu fulani kiko kwenye tovuti au blog yako atatumia fomu hii.

9. Kukosekana kwa kurasa za msingi

Kuna kurasa za msingi zinazopaswa kuwepo kwenye kila tovuti (website) au blog; kurasa hizo ni kama vile: Kutuhusu, Wasiliana nasi, Sera ya faragha, Vigezo na masharti n.k.

Kurasa hizi zitamwezesha mtumiaji kufahamu kuhusu tovuti au blog pamoja na wamiliki wake; pia zitamwezesha mtembeleaji kufahamu njia za kupata msaada au kuwasiliana na wahusika.

Si hayo tu, bali hata sheria na kanuni zinazotawala tovuti husika zitaonekana vyema kwenye kurasa hizi.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha hupuuzi nafasi ya kurasa hizi. Kumbuka! Google hawawezi kutangaza kwenye tovuti au blog ambazo hazina kurasa hizi.

10. Kumuunganisha mtembeleaji bila ridhaa yake

Unahitaji watembeleaji wajiunge kwenye orodha yako ya barua pepe au vitaarifu? Kama jibu ni ndiyo, basi usiwaunge kwa lazima kwani wataichukulia tovuti au blog yako kuwa inaingilia uhuru wao binafsi.

Hakikisha umempa mtembeleaji kitu chenye manufaa kitakachomfanya aone kuwa kuna umuhimu wakujiunga kwenye tovuti au blog yako.

11. Kukusanya taarifa za mtumiaji kwa siri

Kukusanya taarifa za mtumiaji kwa siri bila ridhaa yake ni kosa kisheria; ni lazima ufahamu sera na taratibu zinazotawala faragha ya mtumiaji.

Hivyo kuwa makini unapotaka kukusanya taarifa kama vile jina, barua pepe, umri, jinsia, aina ya kifaa alichotumia, anwani mtandao n.k. Hakikisha mtumiaji wa tovuti au blog yako anafahamu wazi aina ya taarifa unazokusanya pamoja na matumizi yake.

12. Uandishi duni

Uandishi wa kwenye tovuti siyo sawa na ule wa kwenye kitabu au andiko la chuo kikuu. Hivyo ni muhimu ukajifunza uandishi bora na rafiki kwa wasomaji pamoja na injini pekuzi (search engines). Unaweza kuhakikisha haya yafuatayo:

 • Aya na sentesi fupifupi.
 • Matumizi ya mishale na namba (kama ilivyotumika hapa)
 • Matumizi mazuri ya vichwa (H1-H6)
 • Matumizi mazuri ya viunganishi na maandiko pendekezwa.

13. Kosa la kutumia viunganishi vilivyojificha

Inawezekana unataka kuweka kiunganishi mahali ambapo mtembeleaji wa tovuti au blog yako atakibonyeza bila yeye kujua; jambo hili ni baya kwani linakiuka kanuni za kuheshimu matakwa ya watembeleaji.

Hakikisha hufanyi kosa hili kwani hata injini pekuzi kama Google zinasisitiza kuepuka swala la kuficha viunganishi.

14. Kutozingatia kanuni za uboreshaji wa injini pekuzi (Search Engine Optimization -SEO)

Watu wengi wanaanzisha tu blog na tovuti bila kujifunza wala kufahamu umuhimu wa uboreshaji wa injini pekuzi. Uboreshaji wa injini pekuzi ni muhimu kwani utafanya tovuti au blogu yako ionekane kwa watembeleaji. Hivyo hakikisha unafanya uboreshaji wa injini pekuzi jinsi ipasavyo. Unaweza kuzingatia haya:

 • Chagua mada nzuri ya kuandika.
 • Epuka kunakili makala ua maudhui kutoka kwenye blog au tovuti nyingine.
 • Andika kwa uandishi mzuri ambao unasomeka bila shida.
 • Tumia picha vizuri.
 • Andika makala au chapisho lenye urefu wa kutosha.
 • Weka taarifa za meta kwenye kila ukurasa (Maelezo ya ukurasa pamoja na kichwa.) Ikiwa unatumia WordPress unaweza kutumia Yoast SEO itakusaidia sana.

15. Matumizi ya maandishi yanayochezacheza

Maandishi yanayochezacheza (blink) yamepitwa na wakati toka miaka ya 1990, hivyo kutumia maandishi haya hakumsaidii mtumiaji kwa njia yoyote bali humfanya aone tovuti yako ni ya kizamani. Kumbuka kuwa vivinjari mbalimbali havitambui tena mfumo wa maandishi haya.

16. Matumizi makubwa ya teknolojia ya flash

Flash ni teknolojia ya kuweka video, picha, na sauti kwenye tovuti. Kwa kiasi kikubwa ina changamoto nyingi na imeshapitwa na wakati.

Matumizi ya teknolojia ya flash hufanya tovuti ifunguke kwa shida pamoja na kumuweka mtumiaji katika hatari ya kudukuliwa na wadukuzi wanaolenga teknolojia hii.

Inashauriwa kuepuka kosa hili la kutumia flash na badala yake utumie teknolojia ya HTML5

17. Mfumo duni wa viunganishi (menu and navigation)

Mfumo wa viunganishi (menu) ni muhimu sana kwenye tovuti yako, hivi humwezesha mtumiaji kuhama kutoka eneo moja la tovuti au blog yako hadi lingine.

Ni vyema ukahakikisha mpangilio na mfumo wa viunganishi katika tovuti yako umekaa vizuri na unaeleweka.

18. Matumizi mabaya ya rangi

rangi
Tovuti ya Pennyjuice imetumia rangi mbaya.

Watu wengi wana tatizo la kuchagua rangi hasa wanaume, hivyo ni vyema ukafahamu maana na ubora wa rangi kabla ya kuitumia kwenye tovuti au blog yako.

Hebu fikiri blog au tovuti yenye rangi nyekundu asilimia 98, je utaweza kuisoma vizuri? Naamini hutoweza; hivyo ni muhimu kuhakikisha unachagua rangi za tovuti au blog yako kwa makini.

19. Matumizi mabaya ya Javascript

Javascript ni lugha ya kompyuta inayotumika kutengenezea tovuti; lugha hii hufanya kazi mbalimbali kama vile kufanya tovuti kubadilika badilika kutokana na hali au tendo.

Javascript ni lugha muhimu katika utengenezaji wa tovuti na blog, lakini ni muhimu ikatumiwa kwa kiasi na usahihi, kwani matumizi mabaya ya Javascript yataifanya tovuti yako isifanye kazi vyema kwa watumiaji wengi. Kumbuka kuwa siyo vivinjari vyote vya watumiaji vitaweza kusoma lugha hii.

20. Matumizi ya pop up na madirisha mapya ya kivinjari

Popup ni teknolojia ya kufungua vidirisha au viboksi ambavyo huingilia kati kile anachokifanya mtumiaji wa tovuti husika.

Mara nyingi pop up humlazimisha mtumiaji kufanya kile kinachoonekana kwenye pop up kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli au lengo lake.

Matumizi ya pop up pamoja na madirisha mapya ya kivinjari huingilia matakwa au alengo la mtumiaji; hivyo humfanya aondoke kwenye tovuti au blog yako kwani inaonekana kumvamia.

21. Kumlazimisha mtembeleaji kufanya vitu

Ikiwa unalipwa kwa njia ya watembeleaji kubofya picha au kitu fulani kwenye tovuti au blog yako, hakikisha huwalazimishi kufanya hivyo ili upate pesa.

Watembeleaji wakibaini hili hawatakuja tena kwenye tovuti au blog yako kwani wataona kuwa unataka kuwatumia kuzalisha pesa na sio kuwapa kile wanachokihitaji.

22. Kuto kuzingatia lengo

Lengo ni muhimu sana kwenye kufanikisha jambo lolote. Tovuti na blog nyingi hufa kutokana na kukosa lengo; leo unaandika elimu, kesho siasa, keshokutwa habari, siku nyingine udaku, siku nyingine miziki n.k

Huku ni kukosa lengo na kwamwe hutoweza kufanikiwa kama hutoacha kosa hili la kukosa lengo. Bainisha unataka uandike nini, kwa ajili ya nani na kwa ajili ya nini.

23. Kuteka au kumzuia mtembeleaji

Nimeona baadhi ya watu wakifikiri kuwa kumzuia mtembeleaji kuondoka au kumlazimisha kukaa kwenye tovuti au blog zao ndiyo kuzalisha faida zaidi.

Ni kosa kuteka kivinjari au kifaa cha mtumiaji ili asiondoke kwenye tovuti yako.

Hakikisha mtembeleaji mwenyewe anaona sababu ya kuendelea kukaa kwenye tovuti yako na si kwa kumlazimisha.

24. Kuto zingatia kufunguka kwenye vifaa mbalimbali

Hivi leo asilimia kubwa ya watumiaji wa mtandao wanatumia simu za mkononi. Hivyo ni muhimu kuhakikisha tovuti au blog yako inafunguka vyema kwenye vifaa vyote na si kompyuta pekee.

25. Kutumia web host mbaya

Kuna mahali ambapo taarifa au maudhui ya tovuti fulani hukaa; eneo hili ndilo huitwa web host. Kutokana na ukosefu wa uelewa pamoja na kukwepa gharama watu wengi wamejikuta wakitumia host duni ambazo huathiri tovuti zao kwa kiasi kikubwa.

Kumbuka host mbaya zina virusi, wadukuzi, hazipatikani wakati wote, zina kasi ndogo n.k Unaweza kuzingatia mambo haya wakati wa kuchagua web host

 • Hakikisha inapatikana wakati wote (Uptime 99.9%)
 • Hakikisha inaulinzi madhubuti.
 • Hakikisha inahuduma nzuri kwa wateja (Saa 24).
 • Hakikisha wana huduma za kisasa na unazozihitaji.
 • Hakikisha wanaelezwa vyema na watumiaji wengine (Reviews).
 • Hakikisha gharama na njia zao za malipo zinaeleweka vyema.

Kwa kufanya hivi utakuwa umechagua web host nzuri ambayo haita athiri utendaji kazi wa tovuti yako. Fahamu hili tunapendekeza utumie Smart Host UK ni nzuri sana.

Neno la Mwisho:

Karibu kila mtu anaweza kutengeneza tovuti au blog lakini siyo wote wanaoweza kutengeneza tovuti bora. Hakikisha kama unapenda kuwa na tovuti au blog nzuri basi unaepuka makosa tajwa hapo juu. Ikiwa pia unahitaji tovuti au blog ya kisasa na bora kabisa kwa bei nafuu unaweza kuwasiliana na Fahamuhili.com (fahamuhili[at]gmail.com).

Je umeyaepuka makosa haya kwenye tovuti au blog yako? Naamini pia una swali au maoni kuhusu makala hii; tafadhali tuandikie hapo chini.

Karibu pia ufuatilie ukurasa wetu wa Facebook ili ufahamu mengi zaidi; usisahau pia kuwashirikisha wengine makala hii.

 

2.3 6 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

4 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
julius
julius
6 years ago

so great bro keep it up kama tutaweza wasiliana itakuwa poa my namba is 0759442950 julius

Posiani
Posiani
3 years ago

Nimeipenda Mada yako, Ubarikiwe sana ikiwezekana tuwasiliane nafikiri nitapata huduma kwako 0674393539

4
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x