Faida 19 za Kula Maharage Kiafya - Fahamu Hili
Tuesday, June 6Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Faida 19 za Kula Maharage Kiafya

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Maharage

Maharage ni chakula ambacho watu wengi hukichukulia kama chakula cha hadhi ya chini kisichokuwa na manufaa kiafya. Watu wengi huchukulia vyakula kama vile nyama na samaki kuwa ni vya kitajiri wakati maharage yakichukuliwa kuwa ni chakula cha kimaskini.

Huu ni upotoshaji, kwani maharage yana faida nyingi sana mwilini ambazo watu wasiokula maharage wanazikosa.

Kwa kuwa lengo letu ni kukupa maarifa, basi karibu ufuatilie makala hii ili uweze kufahamu faida 19 za kula maharage.

1. Hupunguza lehemu (cholesterol)

Moja kati ya vyakula vinavyopunguza lehemu mwilini ni maharage. Nyuzinyuzi zinazopatikana kwenye maharage hujishikiza na lehemu ziwapo tumboni na kuzuia lehemu zaidi kufyonzwa mwilini.

2. Huzuia saratani

Maharage ni chakula chenye madini ya manganese pamoja na vitamini K ambavyo vyote kwa pamoja huzuia kuharibika kwa seli kunakosababisha saratani.

3. Huboresha afya ya ubongo

Kemikali ya thiamine pamoja na vitamini K zinazopatikana kwenye maharage husaidia katika kuboresha afya ya ubongo.

4. Hutawala kiwango cha sukari mwilini

Maharage yana nyuzi nyuzi ambazo hupunguza kiwango cha metaboli cha wanga (carbohydrates) mwilini. Kwa kufanya hivi huwezesha kutawala kuongezeka kwa kiwango cha sukari hasa baada ya kula chakula.

Maharage pia yana protini ambayo husaidia kupunguza kiwango cha sukari mwilini.

5. Huongeza nguvu za mwili

Kuwepo kwa madini ya chuma pamoja na manganese kwenye maharage kunayafanya kuwa na nafasi kubwa katika kuongeza nguvu za mwili.

Madini haya ni muhimu sana katika kuuongezea na kuupa mwili nguvu.

6. Huimarisha mifupa

Madini ya calcium pamoja na manganese ni muhimu sana kwa ajili ya afya ya mifupa. Maharage ni chanzo kimojawapo kizuri cha madini haya.

7. Huboresha ngozi

Maharage husaidia michakato ya metaboli ya asidi ya amino, gluconeogenesis, neurotransmitter synthesis, histamine synthesis, asidi ya mafuta (fatty acids), lipids and hemoglobin synthesis kwenda vizuri.

Ikumbukwe kuwa hivi vyote vina nafasi kubwa katika kuboresha afya ya ngozi.

8. Huboresha afya ya moyo

Aina nyingi za maharage zina vitamini B9 (folate au folic acid) ambayo ni muhimu kwa ajili ya afya ya misuli ya moyo.

9. Huboresha afya ya macho

Madini ya zinc yanayopatikana kwenye maharage ni muhimu sana kwa ajili ya afya ya macho. Hivyo ulaji wa maharage mara kwa mara utaboresha afya ya macho yako.

10. Huboresha uwezo wa kumbukumbu

Kama nilivyotangulia kusema kuwa maharage huboresha afya ya ubongo, uwezo wa kumbukumbu huboreshwa pia kupitia ulaji wa maharage.

Vitamini B1 inayopatikana kwenye aina mbalimbali za maharage hukabili ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (Alzheimer’s na dementia).

11. Huondoa sumu mwilini

Vyakula vingi vya viwandani huhifadhiwa kwa kutumia vihifadhi vyenye sulphites; Sulphites inapozidi mwilini ni sumu. Hivyo basi kemikali ya molybdenum inayopatikana kwenye maharage inasaidia kuondoa sumu ya sulphites mwilini.

Soma pia: Njia 12 za Kuondoa Sumu Mwilini

12. Hukabili shinikizo la damu

Kama tulivyoeleza kwenye makala nyingine, potassium, magnesium pamaoja na protini husaidia sana kukabili shinikizo la juu la damu. Maharage hukabili shinikizo la damu kwa kuwa ni chanzo kizuri cha potassium, magnesium pamoja na protini.

13. Hupunguza uzito

Vyakula kama maharage vina nyuzinyuzi zinazokuwezesha usihisi njaa mapema, hivyo kuepuka kula mara kwa mara na kusababisha kuongeza uzito wako.

Ikumbukwe pia maharage ni chakula ambacho kina kiwango kidogo cha mafuta (fat), hivyo hakisababishi uzito mkubwa wa mwili.

14. Husaidia kutibu tatizo la kutokupata choo

Kama nilivyoeleza kwenye hoja zilizopita, maharage ni chakula chenye nyuzinyuzi kwa wingi; ikumbukwe kuwa vyakula vyenye nyuzinyuzi ni tiba bora ya tatizo la kutokupata choo.

15. Husafisha tumbo

Wakati baadhi ya watu wakiyachukulia maharage kama kitu kinachovuruga tumbo, maharage yana nafasi kubwa kwenye afya ya tumbo.

Utafiti uliofanyika ulibaini kuwa kula maharage kwa kiasi cha kutosha kutasafisha tumbo lako na kukukinga na maradhi ya saratani ya utumbo (colon cancer).

16. Husaidia kukabili maradhi ya asthma

Utafiti uliofanyika ulibaini kuwa kuna uhusiano kati ya upungufu wa madini ya magnesium na kutokea kwa maradhi ya asthma. Kutokana na maharage kuwa na kiwango kizuri cha madini ya magnesium, basi yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukabili maradhi haya.

17. Huboresha na kukomaza seli nyekundu za damu

Virutubisho vilivyoko kwenye maharage husaidia katika maendeleo na ukomavu wa seli nyekundu za damu.

18. Huzuia kuzeeka mapema

Kuzeeka mapema? Ndiyo, kutokana na maharage kuwa na kemikali zinazozuia kuchakaa kwa seli za mwili, yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuzuia kuzeeka mapema.

19. Huboresha afya ya kucha na nywele

Biotin, madini ya chuma pamoja na protini vinavyopatikana kwenye maharage vina nafasi kubwa katika kukupa kucha imara pamoja na nywele zenye afya njema.

Neno la mwisho

Je bado huoni umuhimu wa maharage katika afya ya mwili wako. Anza kula maharage uboreshe afya ya mwili wako sasa. Ikizingatiwa kuwa maharage ni chakula kinachopatikana kwa bei rahisi tofauti na vyakula vingine kama vile nyama na samaki, hivyo huna kisingizio chochote.

Je una swali au maoni? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kujiunga nasi kwa barua pepe au kwa kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

3.8 4 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
guest

4 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Godlisten Benedict
Godlisten Benedict
4 years ago

Mungu awabariki kwa utafiti wenu

Kornelio Maanga
Reply to  Godlisten Benedict
4 years ago

Nashukuru sana kwa kutembelea blog yetu ya Fahamuhili; tunashukuru pia kwa maoni yako mazuri. Karibu sana Fahamuhili.com

Dickson
Dickson
3 years ago

Asanteni sana.

Kornelio Maanga
Reply to  Dickson
3 years ago

Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com

4
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x