Namna ya Kuwa Mzungumzaji Hamasa (Motivational Speaker) - Fahamu Hili
Thursday, February 22Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Namna ya Kuwa Mzungumzaji Hamasa (Motivational Speaker)

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Mzungumzaji hamasa

Ninapotaja wazungumzaji hamasa (Motivational Speakers) naamini unafahamu kuwa ni watu wanaowasaidia watu kuendeleza na kuwezesha maono au utoto wao wa ndani ili watu husika waweze kufanikiwa. Mzungumzaji hamasa anaweza kuzungumzia mada yoyote ile kulingana na uzoefu wake. Wengi hutamani kuwa wazungumzaji hamasa lakini wameshindwa kujua waanzie wapi. Jambo la msingi katika uzungumzaji hamasa ni shauku yako ya ndani katika mada unayotaka kuizungumzia. Kuwa mzungumzaji hamasa kunahitaji kubaini mada na walengwa wa mada yako bila kusahau kunoa uwezo wako wa kuzungumza mbele ya watu pamoja na kuielewa vyema mada husika.

Kama unatamani kuwa mzungumzaji hamasa, fuatilia hoja jadiliwa hapa chini kwa makini ili sasa uweze kuwa mzungumzaji hamasa.

1. Bainisha mada utakayozungumzia

Huwezi kuzungumza bila kuwa na mada; ni lazima uwe na mada moja au kadhaa utakazozizungumzia wewe kama mzungumzaji hamasa. Zingatia haya yafuatayo wakati wa kubainisha au kuchagua mada:

  • Chagua mada unayoipenda.
  • Chagua mada unayoielewa vyema au ambayo uko tayari kujifunza kwa kina kuihusu.
  • Angalia uhitaji; siyo mada zote zinahitajika; mada kama vile maswala ya vita na ulinzi; tiba na utunzaji wa mazingira ni dhahiri zitakuwa na mvuto mdogo.

Unapobainisha mada utakayokuwa unaizungumzia, inakufanya kujiandaa vyema na kujenga uzoefu katika mada au eneo husika.

2. Fanya ujumbe wako uwe na tija

Wapo wazungumzaji hamasa wengi lakini si wote wanaotoa ujumbe wenye tija. Hivyo soma na fanya utafiti wa kina kuhusiana na yale unayoyazungumzia; hakikisha unatoa vitu vyenye tija kwa wale wanaokusikiliza au kukutazama. Epuka kujaza nafasi kwa maneno matupu yasiyokuwa na msaada wowote kwa msikilizaji au mtazamaji. Kipimo kizuri katika hili ni kuweza kumfanya msikilizaji wako aweke katika matendo yale unayoyazungumza kwa kuwa ameona yana maana kwake.

3. Kuwa mzoefu

Uzoefu ni jambo muhimu katika kazi au taaluma yoyote. Uzoefu ni maarifa au uelewa uliopotikana katika eneo au nyanja fulani kwa kutegemea muda. Hivyo basi ili uwe mzoefu katika uzungumzaji hamasa ni lazima ufanye mazoezi mara nyingi kadri uwezavyo ndani ya muda mrefu. Jitahidi kushiriki katika semina na mafunzo mbalimbali ili kujenga uwezo wako katika uzungumzaji hamasa. Ni muhimu pia kutazama watu wengine ambao ni wazoefu katika uzungumzaji hamasa ili ujifunze mambo kadha wa kadha kutoka kwao.

4. Elewa hadhira

Ni vyema kuelewa hadhira yako ili uweze kuandaa maudhui yatakayowalenga vyema. Ni vyema kujua kama unazungumza na wazee, vijana, watoto, wanawake, wanaume n.k ili uweze kuwalenga kwa upekee zaidi. Kwa mfano mada za mahusiano mara nyingi hupenda na vijana na watu wa umri wa kati lakini si wazee. Hivyo kuielewa hadhira yako kutakuwezesha kujiandaa vyema na kuwa mzungumzaji hamasa bora anayemudu hadhira yake vyema.

5. Jifunze kuzungumza mbele ya watu

Mzungumzaji hamasa anahitaji maarifa mbalimbali; lakini maarifa ya pekee anayoyahitaji ni njia bora za kuzungumza mbele ya watu. Ikiwa mzungumzaji hamasa atakosa maarifa haya, ni wazi kuwa hataweza kuwasilisha mada yake vyema kwa hadhira lengwa.

Unaweza kusoma makala hii juu ya kujenga uwezo wa kuzungumza mbele ya watu: Njia 10 za Kujenga Uwezo wa Kuzungumza Mbele ya Watu.

6. Rekodi hotuba zako

Jizoeze kurekodi hotuba yako kwani itakuwezesha kusikiliza unavyowasilisha mada husika; pia itakuwezesha kutunza masomo au mada husika kwa ajili ya mahitaji mengine ya sasa na ya baadaye. Unaweza kutunza rekodi zako na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii kama vile Youtube, Facebook, Twiter au hata kwenye blogu au tovuti yako kama unayo. Kwa kufanya hivi utaweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa kupitia makala zako ulizozirekodi na kuziweka kwenye mtandao.

7. Fanyia mazoezi uandishi wako

Mara nyingi wazungumzaji hamasa pia ni waandishi. Hivyo ni muhimu ukajifunza mbinu bora za uandishi ili uweze kuandika makala au masomo bora yenye tija kwa wasomaji. Kumbuka siyo lazima uandike vitabu; unaweza kuandika hata makala kwenye mitandao ya kijamii, tovuti au blog kama hii unayoisoma.

Soma pia: Mbinu 7 za Kuwa Mwandishi Bora.

8. Fikiri kuhusu vifaa

Ni muhimu kuandaa vitendeakazi utakavyovitumia katika kazi yako. Uzungumzaji hamasa unahitaji vifaa kama vile Kompyuta, vipazasauti, projekta n.k. ambavyo kama huna namna nyingine ya kuvipata inabidi uwe na vyako mwenyewe. Hivi vitaongeza ufanisi katika kazi yako; pia vitakufanya ufanye kazi kisasa zaidi.

9. Tafuta ukumbi mzuri

Kama ilivyo kwa vifaa, pia utahitaji ukumbi wa kufanyia kazi zako. Wazungumzaji hamasa wengine huandaliwa kila kitu wao ni kuja na kuwasilisha mada yao tu lakini wengine inabidi waandae wenyewe. Hivyo ni muhimu kuchagua ukumbi ambao ni tulivu na unafaa kwa hadhira yako uliyoialika kukusikiliza.

10. Jitangaze

Mzungumzaji hamasa naye anahitaji kujitangaza? Ndiyo, mzungumzaji hamasa naye anahitaji kujitangaza kupitia njia mbalimbali kama vile redio, televisheni na hata mtandao wa intaneti. Kama una bajeti ngumu, unaweza kutumia njia rahisi na nafuu za kujitangaza kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twiter, Instagram n.k. Kwa kufanya hivi utafahamika zidi, utapata kazi nyingi zaidi na kuwafikia watu wengi zaidi.

11. Fuatilia mabingwa wengine

Ni jambo zuri sana kujifunza kwa waliokutangulia. Kutoka kwao utafahamu haya yafuatayo:

  • Walianzaje.
  • Wanakabiliana vipi na changamoto.
  • Wamewezaje kuwa juu kuliko wengine.
  • Wanajiandaa vipi n.k.

Kwa kufanya hivi itakuwa ni rahisi sana wewe kusogea mbele, kwani kuna watu wanaokupa hamasa katika lengo lako la kuwa mzungumzaji hamasa bora.

12. Pokea mrejesho

Wazungumzaji hamasa wengi hawajui nguvu iliyo ndani ya mrejesho wa hadhira zao. Ni vyema ukafahamu hadhira yako inataka nini na inapendekeza wewe ufanye nini. Kama ni mambo ya kuongeza basi yaongeze; ikiwa ni ya kupunguza basi yapunguze ili uweze kukidhi haja yao vyema. Unaweza kupokea mrejesho kwa kutoa nafasi mwishoni unapomaliza kuzungumza au kueleza jambo ili kama kuna yeyote mwenye swali au maoni basi atoe.

Hitimisho

Naamini umebaini kuwa mzungumzaji hamasa ni jambo linalowezekana kama utachukua uamuzi wa kufanyia kazi hoja tajwa hapo juu. Naamini utazingatia maandalizi pamoja na kufanya mazoezi ya kutosha huku ukijifunza kutoka kwa wengine, ili uweze kufikia lengo lako.

Je umenufaika kwa makala hii? Je una swali lolote? Tafadhali niandikie maoni na maswali yako hapo chini; kisha washirikishe wengine.

3 6 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x