Misamiati 20 ya Kiswahili Unayoitumia Kimakosa - Fahamu Hili
Friday, April 26Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Misamiati 20 ya Kiswahili Unayoitumia Kimakosa

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Makosa ya msamiati

Ni wazi kuwa watu wengi wamekuwa wakijitahidi kutumia lugha za kigeni kwa
usahihi kuliko Kiswahili. Ni rahisi mtu kuona aibu kufanya makosa katika
lugha kama vile Kiingereza na Kifaransa lakini siyo Kiswahili.

Ni dhahiri kuwa yapo makosa mengi yanayofanywa na wazungumzaji wa lugha ya
Kiswahili kutokana na kutotilia maanani swala la umahiri katika lugha.
Makosa haya yasipotiliwa maanani yanaweza kukufanya uonekane duni katika
uwezo wako wa kutumia lugha.

Yapo makosa mbalimbali ambayo hufanywa na watumiaji wa lugha yakiwemo yale
ya kimsamiati, kimatamshi, kimuundo n.k.

Katika makala hii nitaonyesha misamiati takriban 20 ambayo pengine
unaitumia au inatumiwa vibaya na wazungumzaji wa lugha hasa kutokana na
makosa ya kimsamiati.

1. Lisaa na Masaa

Lisaa na Masaa ni misamiati au maneno ambayo yamezoeleka sana hasa kutokana
na kutumiwa sana kwenye vyombo vya habari.

Mfano:

  • Hotuba ya raisi imetumia takriban lisaa limoja.

  • Michezo ya ligi kuu ilikuwa ya masaa mawili.

Sentensi hizo hapo juu siyo sahihi, kwani hakuna neno lisaa na masaa katika
Kiswahili sanifu. Badala yake sentensi hizi zilitakiwa ziwe kama ifuatavyo.

  • Hotuba ya raisi imetumia takriban saa moja.

  • Michezo ya ligi kuu ilikuwa ya saa mbili.

2. Nona na nenepa

Maneno mengine ambayo yanatumiwa kimakosa ni neno nona na nenepa.

Mfano:

  • Hamisi amenona sana siku hizi.

  • Ng’ombe wangu wamenenepa sana mwaka huu.

Katika sentensi hizi neno nona limetumika vibaya kwani kinachonona ni
mnyama na sio mtu. Vivyo hivyo kinachonenepa ni mtu na sio mnyama. Sentensi
sahihi zilitakiwa ziwe kama ifuatavyo:

  • Hamisi amenenepa sana siku hizi.

  • Ng’ombe wangu wamenona sana mwaka huu.

3. Jangili

Neno jangili hutumiwa vibaya na wazungumzaji wa lugha bila kuzingatia maana
yake halisi.

Mfano.

  • Majangili yamevamia hoteli huko Nairobi.

Maana halisi ya jangili ni mtu anayeuwa wanyama pori bila kibali au bila
kufuata sheria. Hivyo wanaovamia hoteli ni majambazi na si majangili kama
ilivyotumika katika sentensi hiyo hapo juu. Sentensi sahihi ingeweza kuwa:

  • Majambazi yamevamia hoteli huko Nairobi.

4. Mwenyewe na peke yake

Siyo rahisi kubaini utofauti uliopo katika matumizi ya neno mwenyewe na
peke yake usipoyachunguza maneno haya kwa makini.

Mfano:

  • Juma amelima shamba lote peke yake.

(Mzungumzaji anamaanisha Juma alifanya kazi bila kusaidiwa na mtu mwingine)

  • Roza amekuja shuleni mwenyewe.

(Mzungumzaji anamaanisha Roza amekuja shuleni bila kuambatana na mtu
mwingine)

Kwa kutazama mifano hii ukizingatia maana za msingi za wazungumzaji, ni
dhahiri kuwa zimekosewa. Neno “mwenyewe” hutumika kumaanisha bila msaada wa
mtu au kitu kingine; wakati neno “peke yake” linamaanisha bila kuambatana
na mtu au kitu kingine. Hivyo, ni dhahiri kuwa sentesi hizo hapo juu
zimekosewa na zilitakiwa ziwe kama ifuatavyo:

  • Juma amelima shamba lote mwenyewe

  • Roza amekuja shuleni peke yake.

5. Mrahaba

Hili ni neno linalotumika kimakosa hasa katika vyombo mbalimbali vya
habari. Watumiaji humaanisha kiasi kinacholipwa na wawekezaji kwa wale
walioingia nao ubia katika uwekezaji.

Mfano:

  • Serekali imepokea asilimia tano ya fedha kama mrahaba wa madini.

Neno mrahaba si sahihi kwani halitambuliki katika lugha sanifu ya
Kiswahili. Badala yake neno “Mrabaha” ndiyo neno sahihi. Hivyo sentensi hii
ingekuwa:

  • Serekali imepokea asilimia tano ya fedha kama mrabaha wa madini.

6. Uharamia

Neno uharamia ni neno sanifu katika lugha ya Kiswahili lenye maana ya
ujambazi wa kuteka na kupora vyombo vinavyosafiri majini. Lakini neno hili
limekuwa likitumika vibaya tofauti na maana yake halisi.

Mfano:

  • Maharamia wa kazi za wasanii ni lazima washitakiwe.

Sahihi:

  • Wezi wa kazi za wasanii ni lazima washitakiwe.

7. Rambirambi

Rambirambi ni neno lililozoeleka katika jamii yetu hasa katika mazingira ya
msiba. Watu wengi hulitumia neno hili rambirambi wakimaanisha fedha na vitu
vinavyotolewa wakati wa msiba. Maana halisi ya neno rambirambi ni salamu za
pole zitolewazo kwa wafiwa wakati wa msiba. Neno sahihi kwa ajili ya
kumaanisha fedha na vitu vitolewavyo wakati wa msiba ni “Ubani”

Mfano:

  • Waziri alitoa rambirambi za shilingi laki tano kwa wafiwa.

Sahihi ingekuwa:

  • Waziri alitoa ubani wa shilingi laki tano kwa wafiwa.

8. Tongoza

Tongoza au kutongoza ni neno lililopea zaidi katika upande wa mahusiano ya
kimapenzi baina ya mwanamke na mwanaume. Lakini watu wengi hawafahamu kuwa
neno tongoza linaweza kutumiwa katika mazingira mengine. Maana halisi ya
tongoza ni kumshawishi mtu akubaliane na ombi lako. Hivyo sentensi katika
mfano huu hapa chini ni sahihi.

Mfano:

  • Juma anapenda kutongoza wasichana wengi ili wawe wapenzi wake.
  • Pita alimtongoza baba yake ili ampe fedha za matumizi

9. Mdada, Mkaka, Mmama, Mbaba n.k.

Haya ni maneno yaliyozoeleka katika jamii yetu hivi leo. Maneno haya
yametokana na uambishaji usio sahihi wa maneno. Watu wengi bila kujua
wamejikuta wakitumia maneno haya kama maneno yasiyokuwa na dosari yoyote.
Ukweli ni kuwa maneno haya siyo sahihi.

Mfano:

  • Mdada aliyekuja jana ni ndugu yangu.

  • Huyu mkaka anafanya kazi benki kuu.

  • Mmama na Mbaba mmoja tu, ndio waliohudhuria kwenye mkutano.

Sentensi sahihi zingekuwa:

  • Dada aliyekuja jana ni ndugu yangu.

  • Huyu kaka anafanya kazi benki kuu.

  • Mama na baba mmoja tu, ndio waliohudhuria kwenye mkutano.

10. Zingua

Zingua ni neno lililokolea sana kwenye lugha ya mtaani. Wengi hulitumia
neno hili wakimaanisha kusumbua au kuhangaisha. Ukweli ni kuwa maana hii
bado siyo rasmi. Mana rasmi ya neno zingua ni kumsomea mtu dua kutoka
kwenye Kuran ili Mungu amlinde na mabaya yote. Pia maana nyingine ni
kuondoa kuvurugikiwa.

Mfano:

  • Juma mbona unanizingua sana ndugu yangu?

Sentesi sahihi:

  • Juma mbona unanisumbua sana ndugu yangu?

11. Wakilisha na wasilisha

Wakilisha na wasilisha ni maneno sanifu ya lugha ya Kiswahili lakini watu
wengi wamekuwa wakiyatumia kimakosa.

Mfano:

  • Mama amemwasilisha baba kwenye sherehe ya harusi.

  • Wajumbe wamewakilisha michango yote ya fedha za elimu.

Ni dhahiri kuwa, mtu hawasilishwi bali anawakilishwa; pia ni wazi kuwa
fedha haziwakilishwi bali zinawasilishwa. Hivyo sentensi sahihi zingekuwa:

  • Mama amemwakilisha baba kwenye sherehe ya harusi.

  • Wajumbe wamewasilisha michango yote ya fedha za elimu.

12. Fasaa

Neno fasaa limekuwa likitumiwa na baadhi ya watu wakilenga neno fasaha.
Watu wengi wamekuwa wakitumia neno hili bila kujua kuwa siyo neno sahihi.

Mfano:

  • Mimi ni mzungumzaji wa Kiswahili fasaa.

Neno fasaa hapa si sahihi; ni dhahiri kuwa kosa katika neno hili
limechangiwa na makosa ya kimatamshi au athari za lugha mama. Kwa usahihi
neno hili lilitakiwa kuwa fasaha.

  • Mimi ni mzungumzaji wa Kiswahili fasaha.

13. Mwisho wa siku

Kuna maneno mengine ambayo yamechukuliwa tu kutoka kwenye lugha nyingine na
kuingizwa kwenye lugha ya Kiswahili. Maneno “mwisho wa siku” siyo maneno
sanifu kwani yamechukuliwa moja kwa moja toka kwenye maneno ya Kiingereza
“At the end of the day”.

Mfano:

  • Mwisho wa siku utapata faida kutokana na kazi yako.

Sahihi ni:

  • Hatimaye utapata faida kutokana na kazi yako.

14. Mashule na Mahosipitali

Mara nyingi maneno haya pamoja na mengine yanayofanana nayo yametumiwa
katika miktadha mbalimbali bila kubainika kuwa siyo sahihi.

Maneno haya yanatokana na kutengeneza maumbo ya umoja na wingi katika
maneno yasiyokuwa na sifa hiyo.

Mfano:

  • Mashule yote yamejengwa kwa misaada ya wafadhili.

  • Mahosipitalini hakuna dawa za kutosha.

Sentensi sahihi:

  • Shule zote zimejengwa kwa misaada ya wafadhili.

  • Hosipitalini hakuna dawa za kutosha.

15. Utamaduni

Utamaduni ni neno lingine ambalo ni sanifu katika lugha lakini mara
nyingine hutumiwa vibaya. Maana halisi ya utamaduni ni mwenendo wa maisha
unaohusisha asili, mila, desturi, jadi au itikadi inayotawala katika jamii
fulani. Hivyo siyo sahihi kutumia sentesi kama hii.

Mfano:

  • Wasanii hawa wataimba nyimbo za utamaduni.

Sentensi sahihi ni:

  • Wasanii hawa wataimba nyimbo za asili.

16. Tetesi

Maana halisi ya neno tetesi ni taarifa ambazo bado hazijadhibitishwa.
Lakini watu hulitumia neno hili kinyume na maana halisi.

Mfano:

  • Ufisadi uliofanyika kwenye sekta ya madini uliibua tetesi nyingi za
    malalamiko kutoka kwa wahisani.

Sentensi sahihi:

  • Ufisadi uliofanyika kwenye sekta ya madini uliibua malalamiko mengi
    kutoka kwa wahisani.

17. Bawaba na bawabu

Bawabu na bawaba yote ni maneno sanifu ya Kiswahili lakini mara nyingine
hutumiwa vibaya.

Mfano:

  • Bawabu za mlango huu zimeharibika.

  • Nimekwazika kwa sababu bawaba alichelewa kufungua mlango.

Bawaba ni kifaa kiwekwacho kwenye mlango, sanduku au dirisha ili
kuliwezesha kufunguka na kufungwa. Wakati neno bawabu ni mtu au mlinzi
anayekaa mlangoni ili kufungua na kufunga mlango au lango. Hivyo sentensi
sahihi ni:

  • Bawaba za mlango huu zimeharibika.

  • Nimekwazika kwa sababu bawabu alichelewa kufungua mlango.

18. Dhumuni, Pito, Fao

Haya ni maneno yaliyotokana na maneno yasiyokuwa na maumbo ya umoja; hivyo
huwa si maneno sanifu pale yanapowekwa katika maumbo ya umoja.

Mfano:

  • Dhumuni la barua hii ni kukujulia hali.

  • Nina pito gumu sana maishani mwangu.

  • Tutakupa fao lako la uzeeni kwa wakati.

Sentensi sahihi:

  • Madhumuni ya barua hii ni kukujulia hali.

  • Nina mapito magumu sana maishani mwangu.

  • Tutakupa mafao yako ya uzeeni kwa wakati.

19. Kuoga na Kukoga

Kwa namna moja neno “kukoga” linamaana sawa na kuoga lakini kutokana na
neno kukoga kuwa na maana nyingine nyingi; ni vyema kutumia neno kuoga pale
unapomaanisha kujisafisha mwili mzima kwa maji.

20. Usajilii na udahili

Maneno haya yamekuwa yakitumiwa sana na watu wa ngazi za elimu ya juu
pamoja na taasisi zake. Mara nyingi huchanganywa kimatumizi, hivyo
kusabaisha mkanganyiko kwa wasomaji au wasikilizaji. Ni dhahiri kuwa,
maneno haya yana mana tofauti. Udahili ni mchakato wa kumruhusu mtu
kujiunga na chuo au taasisi bada ya kuridhika na sifa zake. Usajili ni
kitendo cha kuingiza kitu au mtu katika orodha maalumu. Hivyo usajili huwa
ndiyo hatua ya mwisho katika mchakato wa kuwapokea wanafunzi chuoni.

Hitimisho

Ni dhahiri kuwa yapo makosa mengi sana yanayofanywa na wazungumzaji wa
lugha ya Kiswahili. Ni wazi kuwa makosa haya husambazwa kwa kasi kubwa
kupitia vyombo vya habari, sanaa za kizazi kipya pamoja na mitandao ya
kijamii. Ukiwa kama mzungumzaji au mwanafunzi wa lugha ya Kiswahili
unaetaka kuwa mahiri katika lugha ni lazima uyaepuke makosa haya. Pia
vyombo vya habari ni lazima viwe mstari wa mbele kujenga lunga na siyo
kubomoa.

Je inafahamu maneno mengine au unaswali ama maoni kuhusu makala hii?
Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe na wengine.

4.1 7 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

6 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
tallian
tallian
6 years ago

nice program

Kornelio Maanga
Reply to  tallian
6 years ago

Asante na Karibu tena Fahamuhili.com.

Zeni liwonga
Zeni liwonga
3 years ago

Neno:chukua na chukulia

Kornelio Maanga
Reply to  Zeni liwonga
3 years ago

Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com

Samuel Wasilwa
Samuel Wasilwa
1 year ago

Asante sana kwa ufafanuzi wa haya maneno

Kornelio Maanga
Reply to  Samuel Wasilwa
8 months ago

Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com

6
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x