Athari 5 za Kutumia Vyombo vya Chakula vya Plastiki - Fahamu Hili
Tuesday, February 27Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Athari 5 za Kutumia Vyombo vya Chakula vya Plastiki

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Vyombo vya plastiki

Plastiki ina nafasi kubwa kwenye jamii ya leo; hutumika kwenye magari, vyombo vya nyumbani, vifaa vya watoto vya kuchezea, simu, kompyuta n.k. Kwa hakika siyo rahisi mtu kumaliza siku nzima bila kutumia kifaa chochote cha plastiki.

Pamoja na nafasi hii kubwa ya matumizi ya plastiki, plastiki imekuwa na athari mbalimbali kwenye afya ya binadamu pamoja na mazingira.

Karibu nikufahamishe madhara au athari 5 zitokanazo na matumizi ya vifaa au vyombo vya chakula vilivyotengenezwa kwa plastiki.

1. Sumu zilizoko kwenye plastiki zinaweza kukufanya uugue

Tafiti mbalimbali zimebainisha kuwa sumu zilizoko kwenye vifaa vya plastiki zinaweza kusababisha maradhi kama vile saratani, maradhi ya kupoteza kumbukumbu, maradhi ya moyo pamoja na kupoteza uwezo wa kuona.

Wataalamu mbalimbali walisisitiza kuwa sumu hizi huyeyuka na kuingia mwilini hasa pale vyombo vya plastiki vinapowekwa vyakula au vinywaji vya moto.

2. Plastiki huathiri afya ya uzazi

Inaelezwa kuwa kemikali kama vile Bisphenol A inayopatikana kwenye vyombo vingi ya plastiki, ina madhara makubwa kwenye afya ya uzazi.

Watafiti wanaeleza kuwa kemikali hii huathiri uzalishaji wa homoni, ukuaji wa watoto pamoja na kusababisha tatizo la kutoka kwa mimba.

3. Hakuna plastiki salama

Mara nyingi baadhi ya wazalishaji wa vifaa vya plastiki hunadi bidhaa zao kwa kueleza kuwa hazina kemikali ya Bisphenol A (BPA), lakini vinaweza kuwa na kemikali nyingine ya Bisphenol S (BPS) ambayo sifa zake zinakaribiana na za BPA.

Hivyo ni muhimu kuwa makini au kuepuka matumizi ya plastiki kwenye chakula kwani watengenezaji wengi siyo waaminifu wala wa kweli.

4. Huongeza unene

Tafiti mbalimbali zimebainisha kuwa matumizi ya vyombo vya chakula vilivyotengenezwa kwa plastiki huongeza unene wa mwili. Hili ni kutokana na kemikali zinazopatikana kwenye plastiki ambazo hubadili seli shina (stem sell) kuwa seli za mafuta.

Inaelezwa pia kemikali za plastiki zikiingia mwilini huingilia mchakato wa metaboli mwilini na kufanya kalori zikusanyike mwilini badala ya kutumika na kuondoka.

5. Huharibu mazingira

Chazo cha picha: Idogs.in
Ng’ombe wakila mifuko ya plastiki kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Ni wazi kuwa vyombo vya chakula au vinywaji vinapokwisha muda wake hutupa kwenye mazingira yanayotuzunguka. Swala hili huathiri viumbe na mimea mbalimbali.

Plastiki zinapokuwa katika mazingira huathiri ukuaji wa mimea, huweza kuliwa na wanyama pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

ndege
Chanzo cha picha: Publicbroadcasting.net
Ndege aliyekufa akiwa amemeza vipande vya vitu mbalimbali vya plastiki.

Neno la mwisho

Ni ukweli suiopingika kuwa plastiki zina matumizi makubwa lakini pia zina athari kubwa kwenye afya zetu na mazingira. Ni vyema ukatumia vyombo vya udongo, kioo, mbao au hata vya alminiamu badala ya plastiki.

Ni muhimu kukumbuka kuwa maradhi mengi hutokana na sumu mbalimbali zinazoingia kwenye miili yetu. Pia ni muhimu kujali uhai na usalama wa vizazi vijavyo kwa kutunza mazingira ili yatutunze.

Soma pia: Njia 12 za Kuondoa Sumu Mwilini.

Je una maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha usisahau kuwashirikisha wengine makala hii. Unaweza pia kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

2.5 2 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x