Athari 8 Kiafya za Dawa za Kuulia Wadudu — Viwatilifu - Fahamu Hili
Tuesday, March 19Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Athari 8 Kiafya za Dawa za Kuulia Wadudu — Viwatilifu

Washirikishe Wengine Makala Hii:

dawa za kuulia wadudu — viwatilifu

Dawa za kuulia wadudu maarufu kama viwatilifu zimetengenezwa kwa lengo la kuangamiza wadudu wanaoharibu mazao au wanaomdhuru binadamu.

Hata hivyo kutokana na sababu kuwa lengo la dawa hizi ni kuangamiza, huathiri pia viumbe hai vingine akiwemo binadamu.

Takwimu kutoka shirika la afya duniani WHO zinabainisha kuwa kuna zaidi ya vifo 220,000 vitokanavyo na athari za sumu zilizoko kwenye dawa za kuulia wadudu—viwatilifu.

Ikiwa unataka kuweka afya yako salama, basi karibu nikushirikishe athari 8 kiafya za dawa za kuulia wadudu — viwatilifu.

1. Husababisha saratani

Watafiti mbalimbali wa maradhi ya saratani wanaeleza kuwa dawa za kuulia wadudu zinachangia kwa kiasi kikubwa kusababisha seli za saratani mara zinapoingia kwenye mwili wa binadamu.

Hatari hii hutokea zaidi pale ambapo mtu anakula vyakula vilivyoathiriwa na sumu za dawa za kuulia wadudu.

2. Huvuruga mfumo wa homoni

Mwili wa binadamu huzalisha homoni mbalimbali zinazowezesha viungo mbalimbali kufanya kazi vyema.

Dawa za kuulia wadudu zinapoingia mwilini huathiri mfumo wa homoni wa binadamu na kuufanya usifanye kazi vyema.

3. Huathiri mfumo wa uzazi

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa matatizo ya uzazi kati ya wanaume na wanawake huchangiwa kwa kiasi kikubwa na athari za dawa za kuulia wadudu.

Inaelezwa kuwa sumu hizi zinapoingia mwilini kupitia matunda au mbogamboga huharibu mfumo wa uzazi na kusababisha ugumba au utasa.

4. Huharibu ubongo

Madawa ya kuulia wadudu — viwatilifu huathiri pia mfumo wa ubongo hasa kwa watu wanaoyapulizia au kukaa nayo karibu kwa muda mrefu.

Maradhi kama vile Mild Cognitive Dysfunction (MCD) ambayo humfanya mtu ashindwe kutambua vyema maneno, rangi au namba huchangiwa kwa kiasi kikubwa na athari za dawa za kuulia wadudu.

5. Huathiri mama mjamzito na mtoto

Mama mjamzito anatakiwa kuchukua tahadhari nyingi sana wakati wa ujauzito ili kulinda afya yake na mtoto aliyeko tumboni.

Matumizi ya viwatilifu ndani ya nyumba au karibu na makazi kwa lengo la kuua wadudu kama vile mbu, chawa, kunguni, au utitiri kunaweza kumwathiri mama mjamzito na mtoto kwa kiasi kikubwa.

Inaelezwa kuwa sumu hizi zinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa bila viungo vyote, kuzaliwa kabla ya wakati au hata kifo.

Soma pia: Madhara 6 ya Kutumia Dawa Bila Ushauri wa Kitaalamu

6. Huharibu viungo muhimu vya mwili

Kumekuwa na taarifa mbalimbali ulimwenguni zikieleza kuwa dawa za kuulia wadudu huharibu viungo muhimu vya mwili kama vile figo na ini.

Utafiti uliofanyika huko India ulibaini kuwa watu wengi waliokufa kutokana na maradhi ya figo waliishi katika mazingira yenye sumu za kuulia wadudu au kula vyakula vyenye mabaki ya sumu hizo.

7. Huathiri mfumo wa upumuaji

Kutokana na watu wengi kutumia dawa za kuulia wadudu bila kuvaa vifaa vya kujikinga, wengi huvuta sumu zilizoko kwenye dawa hizo na kusababisha kuathiri mfumo wa upumuaji hasa mapafu.

Hivyo ili kujikinga na athari hii inashauriwa kuvaa vifaa bora vya kuzuia kuvuta sumu zilizoko kwenye dawa za kuulia wadudu.

8. Huathiri ngozi

Kama ilivyo kwenye swala la kuathiri mfumo wa upumuaji, watumiaji wengi wa dawa za kuulia wadudu hawakingi ngozi zao kwa mavazi au vifaa maalumu vinavyoepusha athari za dawa hizo kwenye ngozi zao.

Ikumbukwe kuwa sumu zilizoko kwenye dawa za kuulia wadudu zinaweza kuingia mwilini kirahisi kupitia ngozi na kusababisha athari nyingi za kiafya.

Hitimisho

Naamini umeona jinsi ambavyo dawa za kuulia wadudu — viwatilifu zinavyoweza kuathiri afya ya binadamu ikiwa hazitatumiwa kwa uangalifu na kwa kufuata kanuni muhimu za matumizi yake.

Ikumbukwe kuwa vifo vingi na matatizo mbalimbali ya kiafya hutokana na mwili wa binadamu kukutana na sumu mbalimbali, hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari.

Soma pia: Njia 12 za Kuondoa Sumu Mwilini

Je wewe huwa unatumia dawa za kuulia wadudu — viwatilifu jinsi ipasavyo?

Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

1.5 2 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Gift benard
Gift benard
3 years ago

Leo nimetumia lakni nasikia mwili kuchoka pia kichwa kuuma

Kornelio Maanga
Reply to  Gift benard
2 years ago

Pole sana; mwone daktari pia wakati mwingine uchukue tahadhari. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x