Sababu 7 za Kwa nini Hutakiwi Kucheza Michezo ya Kubahatisha - Fahamu Hili
Friday, May 24Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Sababu 7 za Kwa nini Hutakiwi Kucheza Michezo ya Kubahatisha

Washirikishe Wengine Makala Hii:
kubahatisha
Chanzo cha picha: https://www.rd.com

Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi au changamoto za maisha watu wengi hutekwa na mambo mbalimbali hasa yale yanayohusu kupata pesa za haraka.

Nilipofanya utafiti mdogo nilibaini kuwa “njia za kupata pesa kwa haraka” pamoja na “njia za kupata utajiri kwa haraka” ni moja kati ya vitu vinavyotafutwa sana na watu kwenye mtandao. Hii inadhihirisha uhitaji mkubwa wa watu kutaka kupata pesa, tena kwa muda mfupi.

Hivyo basi, hili limepelekea watu wengi kutekwa na michezo ya bahati nasibu wakifikiri kuwa inaweza kuwatoa katika matatizo au mahitaji yao ya kifedha.

Haijalishi unacheza au huchezi michezo ya kubahatisha, karibu nikufahamishe sababu 7 za kwanini hutakiwi kucheza michezo ya kubahatisha.

1. Ni biashara

Hakuna mtu atakayetoka China, India au Marekani ili aje Afrika kukugawia mamilioni ya bure kwa njia ya michezo ya kubahatisha ili utoke kwenye umasikini.

Kampuni za michezo ya kubahatisha zinazalisha faida kubwa tena kubwa sana ambayo hufichwa nyuma ya vijizawadi wanavyotoa kwa washindi wa michezo hiyo.

Kwa mfano watu 100,000 wakicheza mchezo mmoja kwa shilingi 20,000 pekee ni sawa na shilingi 2,000,000,000; hebu jiulize kweli katika bilioni 2 watashindwaje kutoa zawadi ya milioni 50 hata mara 5?

Naamini umeona wanavyopata faida kubwa kwenye biashara hii ambayo huwadanganya watu kuwa ni njia ya kuwatoa kwenye umaskini.

Kumbuka kuwa hivi leo biashara mbalimbali za hovyo hujificha kwenye kofia ya kutambulika kisheria na kulipa kodi. Zipo nchi ambazo zimerasimisha biashara za madawa ya kulevya na silaha kwa kigezo cha kutambulika kisheria na kulipa kodi. Hivyo kuwa macho na michezo ya kampuni hizi kwani ni biashara ya kuwahadaa watu watoe pesa zao.

2. Hakuna mifumo inayoeleweka

Michezo hii haina mifumo wazi na inayoeleweka, wanakuambia cheza mara nyingi ushinde lakini hawasemi ni mara ngapi na ni kwanini wanashinda hata waliocheza mara chache.

Michezo hii huendeshwa kwa mfumo wa kompyuta wa kimahesabu ujulikanao kama probability; hivyo mtu yoyote anaweza kushinda au kushindwa.

Kutokana na sababu hii ni bora kuwekeza pesa zako kwenye kitu kingine chenye tija kuliko kuziweka kwenye michezo ya bahati nasibu isiyokuwa na uhakika.

Nimetafiti nikagundua ni afadhali hata spot betting kwani unachozingatia ni kutabiri matokeo kwa usahihi na unashinda.

3. Hukuathiri na kukuteka kisaikolojia

Michezo ya kubahatisha imetengenezwa kwa njia ambayo inawahadaa na kuwateka wale wanaocheza michezo hiyo. Hivyo huwafanya washindwe kuacha au kujitoa maraa baada ya kuanza kucheza hata kama hawashindi.

Kwa mfano michezo hii hukufanya ushinde kiasi kidogo cha fedha baada ya muda fulani ili uamini kuwa utashinda kiasi kikubwa kama utaendelea kucheza. Lakini hii ni mbinu tu ya kukuteka kwani utajikuta umeshacheza sh. 50,000  lakini umeshashinda sh. 5,000 pekee; huoni hapo unaibiwa?

4. Ni upotevu wa pesa na muda

Kuna vitu vingi na miradi mingi ambayo unaweza kuwekeza muda na pesa zako na ukajipatia faida. Kwanini uchezee shilingi kwenye tundu la choo (michezo ya kubahatisha)?

Ni vyema ukawekeza pesa zako au hata ukanunua kitu cha maana ambacho kitakufaa kwenye maisha yako. Unaweza kuwekeza pesa zako kwenye mradi au ukanunua vitu kama vile vyombo na vifaa vya majumbani, vitabu au hata kuwasaidia wahitaji kwa muda na pesa zako.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda

5. Sio suluhisho la uhakika la kifedha

Watu wengi hufikiri kuwa pesa nyingi au zinazopatikana ghafla ndio utatuzi wa matatizo yao. Hebu nikuulize swali, je ulishawahi kuona watu waliokuwa mamilionea lakini leo wanaomba hata ugali wa mchana? Walikuwa na maduka, magari, majumba lakini leo hawana kitu, je hivi vimekwenda wapi?

Pesa ni lazima zikutane na fikra na mikakati sahihi, ukipewa pesa nyingi leo kama huna fikra sahihi hazitakusaidia kitu.

Kwa kuwa pesa za michezo ya kubahatisha huja kwa ghafla bila kujiandaa wala kuzitolea jasho sana, watu wengi wanaopata pesa hizi huzitumia vibaya na kuishia kurudi kwenye umaskini wao.

Hivyo ni kosa kutegemea michezo ya kubahatisha kama chanzo au suluhisho lako la kifedha.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema

6. Husababisha msongo wa mawazo

Hebu fikiri umecheza kwa kuweka pesa zako kila mara lakini wanashinda wengine, je hili litakupa raha? Naamini litakukosesha furaha na kukupa msongo wa mawazo.

Kutokana na michezo hii kutokutabirika wala kuweza kutambua ni nani atakayeshinda ni vigumu kufahamu uhakika wa pesa ulizoweka kama utazipata au utazipoteza.

Soma pia: Njia 10 za Kukufanya Kuwa na Furaha

7. Hukufanya usifikie malengo

Ukiwakuta watu wanaocheza michezo ya kubahatisha utawaona na kuwasikia wakisema mimi nitatoka tuu siku moja nikishinda huu mchezo.

Watu hawa hawafanyi kazi zenye tija bali wao hukaa na kusubiri kushinda mamilioni kadhaa ili watimize ndoto zao.

Hatimae hujikuta hawashindi na hawatimizi ndoto na malengo yao na kuishia kuwa maskini daima. Ni muhimu kufanya kazi kwa bidii kutimiza malengo yako kwani hakuna atakayekuja kukutimizia malengo yako.

Neno la mwisho

Ni muhimu kila mtu akakumbuka kuwa hakuna njia ya mkato ya kupata pesa au kufanikiwa; njia za mkato zina mwisho mbaya tena mbaya sana.

Kwa uzoefu wangu sijawahi kuona watu waliofanikiwa sana duniani kwa kushinda michezo ya kubahatisha, bali nimeona waliofilisika zaidi baada ya kushinda michezo hii kwani walipata pesa bila kujiandaa.

Naamini sasa umejifunza kitu na hutoweka tena michezo ya kubahatisha mbele. Nia yangu haikuwa kupinga biashara za kampuni za michezo hii bali ilikuwa ni kukupa mtazamo tofauti utakaokusaidia.

Je una maoni au swali lolote? Tafadhali andika maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

4.2 15 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

13 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Magreth
Magreth
4 years ago

safi sana K, bila shaka utawasaidia wengi

Rashidi
Rashidi
2 years ago

Safi sana umetufumbua mawazo safi sana………..

Hassan
Hassan
2 years ago

Nashkur saba

Hassan
Hassan
2 years ago

Umenifumbuwa sana

Baraka
Baraka
1 year ago

Kwa upande wangu nakuunga mkono kuna points umeongea nibora ukacheza hizi betting sport ambazo zipo wazi kabisa na uwe nimfatilia aji wa mpira , siyo uweke kubahatisha na uwe na kiwango ,, na usiwe ndio ndio tegemeo lakipato chakoo .

Leonce
Leonce
1 year ago

Dah kwely kabisa kubeti hakufaii

Dyrell
Dyrell
1 year ago

Tahariri bora, asante Kornelio.
Kusoma huku kumenawiri umuhimu wa kujitosa kuwa na malengo maishani mwako. Maisha ya uraibu wa kamari hauleti faida wowote bali ufukara na hali ya maisha duni.Shukrani

13
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x