Mambo 10 ya Kuzingatia Kabla ya Kununua Kiwanja au Ardhi - Fahamu Hili
Friday, September 29Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kuzingatia Kabla ya Kununua Kiwanja au Ardhi

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kiwanja

Ardhi ni rasilimali muhimu ambayo kila mtu anaihitaji kwa namna moja au nyingine. Watu wengi hununua ardhi kwa ajili ya kufanyia shughuli mbalimbali kama vile ujenzi na kilimo. Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa ardhi bado watu wengi wanakumbana na changamoto mbalimbali katika maswala yanayohusu kununua na kumiliki ardhi. Wengi hujikuta wakinyang’anywa ardhi zao, kuharibiwa mali, au wakiingia kwenye migogoro mikubwa ya kisheria.

Ni wazi kuwa zipo sababu mbalimbali zinazosababisha matatizo haya. Fuatilia makala hii kwa makini ili uweze kufahamu mambo 10 ambayo unapaswa kuyazingatia kabla ya kununua kiwanja au ardhi.

1. Ona kiwanja husika mwenyewe

Ni vyema ukafika kwenye eneo la kiwanja husika na kukiona wewe mwenyewe kama kinakuridhisha na kukufaa kwa mahitaji yako. Fahamu mipaka, na vitu vingine vinavyohusu kiwanja kama vile mimea iliyopo, aina ya udongo n.k. Kwa kufanya hivi utaweza kubaini kama kiwanja kinakidhi mahitaji na matumizi yako.

2. Fahamu mmiliki halisi

Matatizo mengi yanayowakumba watu kwenye maswala ya ardhi ni kutokana na kuuziwa ardhi na mtu ambaye si mmiliki halisi wa ardhi. Ni muhimu sana, tena sana, ukamfahamu mmiliki halisi wa ardhi unayotaka kuinunua kabla hujainunua. Kama ardhi imesajiliwa unaweza kwenda wizara ya ardhi ili kufahamu mmiliki halisi.

Pia ni lazima ufahamu kama kiwanja au ardhi kinamilikiwa na wanandoa (matrimonial property) ili upate ridhaa ya familia juu ya kununua kiwanja husika. Mara nyingi watu hasa wanaume huuza viwanja vya familia kwa siri bila kushirikisha familia; jambo ambalo linaweza kukuingiza kwenye mgogoro mkubwa na familia husika. Kwa kumfahamu mmiliki halisi utaweza kuepuka migogoro au kupoteza pesa zako.

3. Epuka madalali

Karibu kila kinachouzwa leo kuna madalali. Madalali hawana cha ziada zaidi ya kutafuta njia za ujanja ujanja za kupata pesa. Kama kiwanja kinauzwa milioni 5 dalali anaweza kukuambia milioni 7 ili apate zake 2. Hivyo ni muhimu kumtafuta mwenye mali halisi ili uzungumze na kupatana naye kuhusu gharama halisi za kiwanja. Kwa kufanya hivi utaokoa pesa zako ambazo zingechukuliwa na madalali.

4. Angalia uwepo wa huduma za kijamii

Uwepo wa huduma za kijamii katika eneo husika ni muhimu sana, lakini watu wengi huwa hawazingatii hili. Ni muhimu kabla hujanunua kiwanja ukaangalia uwepo wa huduma kama vile maji, hospitali, barabara, soko, shule, nyumba za ibada n.k. Hili litakuwezesha hasa kama unataka kuishi eneo husika kupata huduma za kijamii kwa karibu bila shida wala gharama ya ziada.

Barabara ya tope
Barabara mbaya ya tope.

5. Chunguza migogoro ya kisheria

Kutokana na makosa mbalimbali yanayofanyika kwenye maswala ya ardhi, ardhi nyingi sana hivi leo zina migogoro ya kisheria. Ni vyema ukajiepusha kujitumbukiza kwenye kesi na matatizo yasiyokuwa ya lazima kwa kununua kiwanja au ardhi yenye mgogoro wa kisheria. Unaweza kulibaini hili kwa kufanya uchunguzi wa kina kabla hujanunua ardhi husika.

6. Chunguza kama kiwanja kimewekwa rehani

Viwanja na mashamba huwekwa rehani kwa taasisi mbalimbali hasa zile za kifedha. Watu wenye nia mbaya huuza viwanja vilivyowekwa rehani. Kununua kiwanja hiki kutakuingiza kwenye mgogoro na taassisi husika. Na kwa sababu taasisi hii inakihodhi kisheria, hutoweza kukipata kiwanja husika bali unaweza kupoteza fedha zako.

7. Fahamu hali ya kijografia ya eneo

Nimeshuhudia watu wakiuziwa viwanja kwenye mikondo ya maji pamoja na matindiga; hali inayowapelekea kupata adha kubwa wakati wa mvua. Ni vyema ukafahamu hali ya kijografia ya kiwanja au ardhi unayoinunua. Hakikisha mambo yafuatayo:

  • Eneo husika siyo tindiga au kinamasi
  • Eneo husika siyo mkondo wa maji – unaweza ukazolewa na mafuriko hapa.
  • Eneo husika siyo bonde linalojaa maji
  • Eneo husika siyo eneo la magadi
  • Siyo eneo la maporomoko ya ardhi
  • Siyo eneo lenye ardhi inayotitia n.k
Mafuriko
Nyumba zilizozungukwa na maji. Je unaweza kuishi hapa?

Kwa kutazama baadhi ya mambo kama haya ya msingi, utaweza kuhakikisha unanunua eneo zuri na salama kijografia.

8. Chunguza kama kiwanja kipo kwenye mpago au hifadhi maalumu

Kuna maeneo ya ardhi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli maalumu. Maeneo hayo yanaweza kuwa ni ya miradi ya serikali, maeneo ya wazi, hifadhi ya barabara, hifadhi ya wanyama pori, chanzo cha maji au hata ardhi ya kampuni au taasisi fulani. Watu wengi wamenyang’anywa ardhi zao au hata pengine kuharibiwa mali zao kwa kosa la kujenga au kufanya shughuli katika maeneo haya.

Nyumba ikibomolewa.
Nyumba ikibomolewa kutokana na kujengwa sehemu isiyostahili.

Inashauriwa kuchunguza ardhi vyema kabla ya kuinunua ili uweze kubaini maswala haya. Pia unaweza kwenda kwenye ofisi zinazoshughulika na maswala ya ardhi na mipango miji ili kupata taarifa kamili.

9. Fahamu kama kuna mpangaji au mkodishaji

Kuna watu wanakodisha ardhi kwa ajili ya shughuli na miradi mbalimbali kwa kipindi fulani cha muda. Hivyo kabla ya kununua ardhi hakikisha kuwa hakuna mkodishaji au mmepatana naye kwanza. Ni vigumu kumtoa mtu aliyekodisha ardhi na kuilipia kwa miaka kumi kwa kigezo tu kuwa umeinunua. Hivyo kuwa makini na chunguza swala hili kabla.

10. Husisha mwanasheria au taratibu za kisheria

Kutokana na ukosefu wa elimu pamoja na hali ya mazoea, watu hujimilikisha ardhi bila kufuata taratibu za kisheria. Ni lazima ufahamu kuwa ardhi ni kitu kinachomilikiwa kisheria. Hivyo ni lazima makabidhiano au manunuzi ya ardhi yazingatie sheria na kuhusisha ushahidi wa kisheria kama inawezekana.

Unapomhusisha mwanasheria katika manunuzi yako ni wazi kuwa utajiwekea uhakika wa kuwa mmiliki halali kwani umefuata taratibu za kisheria. Zipo taasisi nyingi unazoweza kuziona na ukapata usaidizi wa kisheria bure au kwa bei nafuu.

Hitimisho

Naamini umefahamu mambo kumi ambayo ni muhimu sana ukayazingatia kabla ya kununua kiwanja au ardhi. Ni wazi kuwa matatizo na migogoro mingi huibuka kutokana na kutozingatia maswala tajwa hapo juu hasa kutokana na ukosefu wa elimu na kwenda kwa mazoea. Tambua ardhi ni jambo nyeti, usikubali kuzuzuliwa na bei au maneno ya muuzaji; hivyo ni lazima uwe mwangalifu na ufanye uchunguzi wa kina kabla ya kununua kiwanja au ardhi.

Soma pia: Makosa 8 ya Kuepuka Kabla na Wakati wa Kujenga Nyumba.

Je wewe unayazingatia haya kabla ya kununua ardhi? Je ulishapata tatizo la ardhi? Ulilimalizaje? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza pia kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

4.2 5 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

21 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Musa mapinda
Musa mapinda
5 years ago

Very nice

Raymond Majengo
Raymond Majengo
4 years ago

uko vizuri kijana , Keep it up aisee. Hii website iko very educative

Nassibu
Nassibu
4 years ago

Nashukuru sana , umenielimisha . nataka kununua ardhi Kwa elimu hii itanibidi kuwa makini sana zaid ya sasa

Evian Kamala
Evian Kamala
3 years ago

Kazi nzuri. Ila natamani pia uelezee suluhisho kwa baadhi ya matatizo, maana wasomaji wengi hatuna elimu juu ya ardhi. Mfano, nitajuaje kiwanja kimewekwa rehani, au kimepangishwa…nk. Asante kwa makala hii.

mauli
mauli
3 years ago

Kazi nzuri sana, jitihada zako ni zenye kuthaminiwa

Odan
Odan
3 years ago

Asante kwa ushauri mzuri .Kama nataka kununua ardhi ambayo haijapimwa natakiwa nifuate taratibu zipi? Nifanyaje ili nijimilikishe kiwe Mali yangu?

Peter Felix Sumbizi
Peter Felix Sumbizi
Reply to  Kornelio Maanga
5 months ago

Jina langu naitwa Peter Felix Sumbizi . Kwanza nakupongeza Sana , Sana kwa elimu hii ya masuala mazima kuhusiana na mambo ya kuzingatia katika ununuzi wa ardhi ! Ahsante 🙏 Mheshimiwa . Endelea kutuelimisha Watanzania . MUNGU AKUBARIKI SANA !

Augustine Chavala
Augustine Chavala
2 years ago

Thanks for this

Samwel warento
Samwel warento
2 years ago

Nimeipenda

Wilson Baitani
Wilson Baitani
2 years ago

Ni makala nzuri.

Fredy
Fredy
8 months ago

Ahsanteni kwa darasa zuri

21
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x