
Duka la TECNO lililopo eneo la Milimani City nchini Tanzania.
China ni moja kati ya nchi zenye makampuni mengi yaliyowekeza barani Afrika. Takwimu zinaeleza kuwa zaidi ya kampuni 10,000 za kichina zipo barani Afrika kwa sasa.
Inaelezwa kuwa kampuni hizo zimefanikiwa sana na kujipatia faida kubwa kwa muda mfupi. Takwimu hizo zinaeleza kuwa robo ya kampuni hizo zilirudisha mtaji wake ndani ya miezi 12, wakati asilimia 50 zilitumia takriban miaka mitatu au pungufu kurudisha mtaji wake.
Fahamuhili tunapenda kukupa maarifa, hivyo fahamu kampuni 7 za China zilizofanikiwa sana barani Afrika kwa mwaka 2017.
1. TECNO
Hii ni kampuni ya kuuza vifaa vya kielektroniki, hasa simu kutoka China. Inaelezwa kuwa kampuni hii imefanikiwa kushika asilimia 40 ya soko katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.
Pamoja na ushindani mkubwa kutoka kwa wazalishaji wengine duniani, bado TECNO imeweza kutoa bidhaa za gharama nafuu na zinazopendwa zaidi.
2. Twyford
Twyford ni kampuni maarufu kutoka China inayozalisha vifaa vya ujenzi. Mwanzoni kwa kupitia kampuni ya Sunda, Twyford ilianza kuingiza vigae barani Afrika kutoka nchini China.
Kwa sasa kampuni hii imeshajenga viwanda kwenye nchi mbalimbali barani Afrika na kuajiri maelfu ya wafanyakazi kutoka Afrika.
3. Huawei
Huawei ni kampuni ya mawasiliano na vifaa vya mawasiliano kutoka China. Kampuni ya Huawei imefanya mambo mengi katika kuziongezea uwezo kampuni za mawasiliano za Afrika.
Mnamo mwaka 2015 kampuni ya Safaricom ya Kenya ilihamishia wateja wake wa M-Pesa wapatao milioni 12.8 kwenye miundombinu ya Huawei. Hii ni kwa lengo la kuboresha mawasiliano, uharaka na usalama wa miamala ya pesa.
4. Sunshine Group
Sunshine Group ni mfano wa kampuni ya kichina ambayo ilianza kama kampuni moja na kupanuka kuwa makampuni mengine mengi.
Kampuni hii ilianza nchini Tanzania mnamo mwaka 2012 kama kampuni ya uchimbaji wa madini, lakini sasa imeshaingia kwenye kilimo, uzalishaji na hata usafirishaji.
Kampuni hii iliwekeza takriban dola milioni 100 katika mitambo ya kuchakata dhahabu, mitambo ya kuchakata mazao ya kilimo na mitambo ya kutengeneza kadi za simu na benki.
5. StarTimes
StarTimes ni kampuni maarufu sana barani Afrika inayojihusisha na huduma za televisheni za kulipiwa. Kampuni hii ina wateja wapatao milioni 10 na inahudumu kwenye nchi zaidi ya 30 barani Afrika.
Kwa mfano nchini Tanzania kampuni ya StarTimes imepunguza gharama za televisheni za kulipiwa kwa asilimia 90. Na huko nchini Kenya wamewezesha maeneo ya vijijini kufikiwa na huduma ya televisheni kwa njia ya satelaiti.
6. Bobu Africa
Siyo kila kampuni ya Kichina iliyoko Afrika imewekeza kwenye viwanda au uzalishaji mkubwa. Kampuni ya Bobu Africa ni kampuni iliyoanzishwa na wanandoa wawili wa Kichina ili kuendesha shughuli za utalii.
Waanzilishi wa kampuni hii wamebuni mfumo ambao watalii hutembelea wasaanii na wabunifu wa Kiafrika ili kuwaongezea pato lao.
7. FAW
FAW ni kampuni ya China iliyowekeza zaidi ya dola milioni 50 huko Afrika Kusini katika kiwanda cha kuunganisha magari. Kampuni hii huzalisha zaidi ya magari 5,000 kwa mwaka wakilenga soko la nchi ya Afrika Kusini na nchi nyingine za Afrika.
Mnamo mwaka 2013 iliingia kwenye ushirikiano na kampuni ya Perfection Motors ili kuunganisha na kuuza magari yake nchini Nigeria.
Je una maoni gani kuhusu makala hii? Tafadhali tuandikie hapo chini. Usisahau kuwashirikisha wengine makala hii pamoja na kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.